Thursday 14 January 2016

Kipindupindu Chaitesa Simiyu, Wanne Wafa, 85 Waugua

Kipindupindu Chaitesa Simiyu, Wanne Wafa, 85 Waugua

Tarehe January 14, 2016
kipindupindu
Watu wanne wamekufa wilayani Bariadi mkoani Simiyu kutokana na ugonjwa wa kipindupindu na wengine 85 wameugua na kutibiwa, huku kambi saba zikitengwa kwaajili ya wagonjwa katika wilaya za Busega na Bariadi.
Akizungumzia mlipuko wa ugonjwa huo daktari mwandamizi kitengo cha dharura na maafa wizara ya afya, maendeleo ya jamiii, jinsia, wazee na watoto, Dr Mary Kitambi amesema kufuatia kuongezeka kwa wagonjwa wa kipindupindu imewalazimu kufika mkoani Simiyu ili kuhakikisha wanashirikiana na mkoa katika kutokomeza ugonjwa huo kwa kuihamasisha jamii kuzingatia usafi.
Mwakilishi wa shirika la afya duniani WHO nchini Zambia, Nora Mwemba ambaye ameambatana na watalaam toka wizara ya afya amesema amekuja nchini ili kuongeza nguvu ya utoaji wa elimu pamoja na mahitaji ya dawa kwa wahudumu wa afya ili jamii iweze kuelewa na kuondokana na ugonjwa huo.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Simiyu, Eraston Mbwilo aliyetembelea wagonjwa katika kambi ya Dutwa wilayani Bariadi na Chamugasa wilayani Busega ameagiza kila  kaya inazingatia usafi kwa kunawa kabla na baada ya kula, huku akiwaagiza wakuu wa wilaya ya Busega na Bariadi kukutana kwaajili ya kuweka mpango mkakati wa kudhibiti mlipuko huo.

clouds stream