Friday 29 April 2016

Naibu Spika Azua Gumzo Kwa Kumuita Mbunge ‘ Bwege’

Naibu Spika Azua Gumzo Kwa Kumuita Mbunge ‘ Bwege’

Tarehe April 29, 2016
Naibu Spika wa Bunge  Tulia Ackson.Naibu Spika wa Bunge Tulia Ackson.                                                                       Naibu Spika Tulia Ackson amezua gumzo Bungeni jana  kufuatia  kumuelezea mbunge wa Kilwa Kusini (CUF), Selemani Said Bungara kuwa ni bwege.
 “Na wewe Mheshimiwa Bwege, hebu kaa chini. Usionyeshe ubwege wako hapa,” alisema Dk Ackson kumzuia mbunge huyo asiendelee kuzungumza wakati  wa mjadala.
Kitendo cha kutumia neno bwege kumuelezea mbunge huyo kilisababisha wapinzani wacharuke, na kuibua bungeni kesi ya mtu aliyefunguliwa mashtaka mkoani Arusha kwa kosa la kumuelezea Rais John Magufuli kuwa ni bwege.
Bila ya kuruhusiwa, mmoja wa Wabunge  alifungua kipaza sauti na kusema: “Hatimaye msamiati wa bwege watua bungeni sasa kutumika rasmi. Futa lugha ya kuudhi; bwege bwege.”
Akizungumzia suala hilo Mbunge wa Moshi Vijijini (Chadema), Antony Komu alisema: “Kauli iliyotolewa na Naibu Spika inaonyesha wazi kuwa ni kiongozi anayekiuka misingi, taratibu na kanuni za Bunge. Tazama anatukana watu tu bila kujali jambo lolote, hii si sawa kabisa.”
Naye Mbunge wa Kalenga (CCM), Godfrey Mgimwa alisema Dk Tulia alighafilika wakati akitoa kauli hiyo baada ya kurushiwa maneno mara kwa mara na wabunge wa upinzani, tena bila kufuata kanuni na taratibu za kibunge.
Hivi karibuni  Mkazi wa  Arusha, Isaack Habakuk Emily alipandishwa kizimbani  akikabiliwa na shitaka la kumuita Rais kuwa ni bwege.

clouds stream