Majambazi yavamia kituo cha Polisi na kupora silaha Kilombero
Wimbi la vituo vya Polisi kuvamiwa na kuporwa silaha linazidi kushamili kufuatia kituo kingine cha Polisi cha Mngeta Kilombero mkoani Morogoro kuvamiwa na kundi la Majambazi na kuporwa bunduki aina ya SMG yenye risasi 30.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paul alisema uporaji huo ulitokea usiku wa Februari Mosi ambapo licha ya kupora silaha waliiba pia jenereta, redio, viti, berti ya Gari pamoja na spika ya redio.
Hadi sasa kituo hicho ni cha tatu kuvamiwa ambapo vituo vingine ni Kituo Kikuu cha Polisi Rufiji, Mkoa wa Pwani na Bukombe kuvamiwa na majambazi na kuua polisi wawili na kupora bunduki saba na risasi 60. Mwaka jana majambazi walivamia Kituo cha Polisi Mkamba, wilayani Mkuranga, Pwani na kuua askari mmoja na mgambo wawili kisha kupora bunduki tano na risasi 60, pamoja na tukio la Polisi kuporwa silaha mkoani Tanga.
Kwa upande mwingine Kamanda Paulo alisema baada ya wizi huo askari walianza msako na kufanikiwa kuipata bunduki hiyo na risasi 30, viti vitatu, jenereta na redio vikiwa vimefichwa katika pori la Simbangingile lililopo Mngeta Wilaya ya Kilombero.
Jeshi la Polisi inawashikilia watu watatu kutokana na tukio hilo ambao ni Ramadhani Shewele (20), Hamisi Ahmed (45) na Ignus Shewele (34) wote wakazi wa Nakagulu.