Friday 24 March 2017

Nape Azungumza Chini Ya Ulinzi Wa Polisi

nape
img-20161130-wa0008

Aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye amewashukuru wanahabari kwa ushirikiano wao katika kipindi chote cha mwaka mmoja alichokuwa Waziri mwenye dhamana ya Habari.

Nape ametoa shukrani hizo leo nje ya Hoteli ya Protea, Jijini Dar es Salaam alipokuwa amepanga kukutana na wanahabari kabla ya Kamanda wa Polisi Kinondoni, Suzana Kaganda kumpigia simu mmiliki wa hoteli hiyo na kuzuia mkutano huo na kusema kuwa ameshangazwa na kitendo cha polisi kumuonyeshea bunduki alipokuwa akitaka kuzungumza na wanahabari.

Nape amemshukuru pia Rais Magufuli kwa kumuamini na kumteua katika nafasi hiyo na sasa muda umefika ameona aondoke katika wizara hiyo na kwamba hana kinyongo na uamuzi huo.

Amewataka wanahabari kuendelea kushirikiana vyema na Waziri anayekuja katika Wizara ya Habari, Dkt. Harrison Mwakyembe pamoja na Rais, Dkt. John Pombe Magufuli ili kuzidi kuijenga Tanzania.

Awali Meneja wa Protea Hotel alidai kuwa amepigiwa simu na Kamanda wa polisi Kinondoni kusitisha mkutano wa waandishi wa habari ambao uliitishwa na aliyekuwa Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Nape Nauye na hivyo kumlazimu kuongea akiwa juu ya gari.

Hatahivyo, Kamanda Kaganda alifika eneo hilo na mara baada ya Nape kuagana na waandishi waliokuwa wakitaka aendelee kuzungumza aliitwa katika gari alimokuwa Kamanda Kaganda na kuzungumza kwa dakika chache kasha kurejea katika gari lake na kusema kila kitu kipo sawa.

“Naomba muendelee na shughuli zenu hakuna kitu chochote cha ajabu, huyu alikuwa anapita tukakutana hapa hivyo msiwe na wasiwasi. Mtanisaidia kama mtaondoka eneo hili,” Nape aliwaeleza waandishi wa habari waliokuwa wakipiga kelele kutaka kujua yaliyozungumzwa kati yake na Kamanda Kaganda.

Awali leo asubuhi Rais Magufuli amefanya mabasiliko madogo ya Baraza la Mawaziri kwa kumteua Profesa Palamagamba Kabudi kuwa Waziri wa Katiba na Sheria huku Dkt. Harrison Mwakyembe akiteuliwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

clouds stream