Friday 4 November 2016

Kesi Ya Kwanza Yaanza Kuunguruma Mahakama Ya Mafisadi

nyundo
Gavel and Law BooksV 2

Kesi ya kwanza ya uhujumu uchumi imeanza kusikilizwa rasmi jana na Mahakama ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ikiwahusisha Mtanzania mmoja na raia wa China na mwingine wa India.

Mahakama hiyo maarufu kama ‘Mahakama ya Mafisadi’ inatokana na ahadi za Rais John Magufuli aliyoitoa wakati wa kampeni zake kushughulikia mafisadi nchini.

Kwa pamoja washtakiwa hao wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi wakidaiwa kukutwa na nyavu haramu za kuvulia samaki zilizopigwa marufuku zenye thamani ya zaidi ya Sh7.4 bilioni.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na kesi ya msingi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, lakini wamefungua maombi ya dhamana katika Mahakama hiyo na hivyo kuweka rekodi ya kuwa kesi ya kwanza kusikilizwa.

Hata hivyo, maombi hayo yamewekewa pingamizi na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), akipinga washtakiwa hao kupewa dhamana akidai yamefunguliwa kwenye Mahakama isiyo sahihi.

Pingamizi hilo lilisikilizwa jana na Jaji Rehema Mkuye na baada ya hoja za pande zote alipanga kutoa uamuzi Novemba 14.

Wakati wa usikilizwaji wa pingamizi hilo mvutano mkali wa kisheria uliibuka baina ya upande wa mashtaka na utetezi kuhusu tafsiri ya Mahakama Kuu.

Wakili wa Serikali Mkuu (PSA), Timon Vitalis alidai kuwa sheria inatamka kuwa Mahakama Kuu na siyo Mahakama ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Wakili huyo alidai Mahakama hiyo (ya ufisadi) inakuwa na uwezo wa kutoa dhamana pale kesi ya msingi inakuwa tayari imeshafunguliwa mahakamani hapo.

Hata hivyo, wakili wa washtakiwa hao, Roman Lamwai alipinga hoja hizo akidai Mahakama hiyo ni mahali sahihi kwa mujibu wa tafsiri ya Sheria ya Uhujumu Uchumi kama ilivyofanyiwa marekebisho.

Alisisitiza kuwa hata ukubwa wa gharama zinazohusika katika kesi ni lazima maombi hayo yafunguliwe kwenye Mahakama hiyo yenye jukumu la kusikiliza na kuamua kesi za rushwa na uhujumu uchumi.

Moja ya vigezo vya kesi zinazofunguliwa katika Mahakama hiyo ni kiwango cha fedha za rushwa au uhujumu uchumi kinachohusika ambacho ni kuanzia Sh1 bilioni.

Hata hivyo, DPP anaweza kufungua kesi mahakamani hapo chini ya kiwango hicho kulingana na mazingira maalumu kadri atakavyoona kuwa inafaa.

Katika kesi ya msingi inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Godfrey Mwambapa kwenye shitaka la kwanza washtakiwa Feng na Kerenge wanadaiwa kutenda kosa la uhujumu uchumi kwa kuagiza nyavu haramu nje ya nchi.

clouds stream