Sunday 27 November 2016

Maalim Seif: Sijahusika Kumfukuza Lipumba

Mwenyekiti wa chama cha CUF Prof Ibarahim Lipumba na makamu mwenyekiti wake Maalim Seif.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF, Maalim Seif amesema kuwa yeye sio sababu ya mgogoro uliopo sasa katika chama hicho na wala hajahusika kumfukuza uanachama Lipumba. Amesema CUF kupitia Baraza lake la Uongozi la Taifa liliamua kumfuta uanachama kwa sababu ya kukiuka katiba ya chama hicho.

“Sina ugomvi na Lipumba, sijamfukuza, na niko radhi kufanya nae mdahalo ili aeleze siri ya kujiuzulu na kung’ang’ania uenyekiti wa CUF. Na hata tukipatanishwa haitasaidia kitu sababu, siwezi badilisha, chama ndicho kilichomfukuza kwa kura za wajumbe zaidi ya asilimia 70,” amesema.

Maalim amedai kuwa, Lipumba anatumiwa na baadhi ya watu kuuzima mgogoro wa uchaguzi uliotokea visiwani Zanzibar mwaka jana.

“Mgogoro huu wa CUF ni muendelezo wa hujuma zinazohusiana na kuzima harakati za kudai haki Zanzibar, ndio maana Lipumba analindwa na vyombo vya dola kuuendeleza mgogoro huu ili CUF ishindwe fuatilia mgogoro wa uchaguzi Zanzibar na kwamba wakubwa waonekane hawakukosea,” ameongeza.

Kauli ya Maalim inakuja wakati kukiwa bado na mgogoro unaoendelea ndani ya CUF kuanzia ngazi ya kata hadi taifa, ambapo viongozi waandamizi wa chama hicho ambao ni Katibu Mkuu Maalim Seif Hamad na aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho aliyefutwa uanachama wameendelea kusigana na kupelekea kufunguliwa kwa kesi mahakamani dhidi ya Lipumba, Msajili wa Vyama vya Siasa na wengine.

Hivi karibuni Lipumba akiwa katika mkutano wake wa ndani na baadhi ya viongozi wa Kamati ya Utendaji ya CUF wilaya ya Temeke, alidai kuwa Maalim na wafuasi wake wanapanga mikakati ya kukiuza chama na kwamba anahonga baadhi ya viongozi wa CUF kuanzia kata ili wamkatae kwa madai kuwa yeye ni kikwazo kwa Maalim kukiuza chama hicho.

clouds stream