Wednesday 23 November 2016

Serikali Kula Sahani Moja Na Waajiri Wanaonyanyasa Wafanyakazi


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Serikali imesema kuwa haitawavumilia waajiri ambao hawatoi mikataba ya ajira kwa wafanyakazi wao na amewaonya waache tabia hiyo mara moja.

Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipokuwa akifungua Mkutano Mkuu wa Sita wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) katika ukumbi wa Mwalimu Julius K. Nyerere ulioko Chuo cha Mipango, nje kidogo ya mji wa Dodoma.

Amesema kifungu cha 14 cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na. 6 ya mwaka 2004 kinaelekeza aina mbalimbali za mikataba inayotakiwa kutumika kuajiri wafanyakazi.

“Kisheria mwajiri anao wajibu wa kuhakikisha kila mtumishi wake ana mkataba wa kazi kwa maandishi,” amesema.

Kuhusu wafanyakazi kuwekwa ndani kiholela, kunyanyaswa, kushushwa vyeo na kusimamishwa kazi na wanasiasa, Waziri Mkuu amesema Serikali chini ya uongozi wa Dkt. John Pombe Magufuli itaendelea kuzingatia utawala wa sheria na kanuni za utawala bora ili kuhakikisha kuwa haki za wafanyakazi zinalindwa ipasavyo.

“Kimsingi watumishi wanasimamiwa na mamlaka za kinidhamu na sheria mbalimbali ambazo hazina budi kuangaliwa kwa pamoja kabla ya kuchukua hatua. Ninawaagiza viongozi wenzagu wa kisiasa na walioko katika wizara na taasisi zote za Serikali, mikoani, wilayani, kwenye idara za Serikali na Halmashauri wazingatie utawala wa sheria wakati wa kushughulikia masuala mbalimbali yanayohusu wajibu na haki za wafanyakazi,” ameongeza.

clouds stream