Sunday 27 November 2016

Rais Wa Zambia,Chad Uso Kwa Uso Na Rais Magufuli

Rais John Pombe Mafgufuli akimpokea mgeni wake Edgar Lungu uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Rais John Pombe Mafgufuli akimpokea mgeni wake Edgar Lungu uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Rais wa Jamhuri ya Zambia Mhe. Edgar Chagwa Lungu amewasili nchini Tanzania kwa ziara ya kiserikali ya siku 3 kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.

Rais Lungu amepokelewa na mwenyeji wake Rais Magufuli na kulakiwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, Mabalozi wanaowakilisha nchi mbalimbali nchini humo pamoja na wananchi.

Akiwa uwanjani hapo Rais Lungu amepokea heshima ya kupigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride rasmi lililoandaliwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ).

Rais Lungu ataendelea na ziara yake ambapo pamoja na kutembelea miradi ya ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia ikiwemo TAZARA na TAZAMA, atafanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake Rais John Pombe Magufuli, atashuhudia utiaji saini mikataba mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia na jioni atahudhuria dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa na Rais Magufuli kwa ajili yake Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Chad Mhe. Idriss Deby Itno naye amewasili nchini Tanzania kwa ziara kikazi ya siku 2. Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.

Rais Idriss Deby Itno akiwa na Mkewe Mama Hinda Deby amepokelewa na mwenyeji wake Rais Magufuli na kisha kulakiwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa na wananchi.

Rais Magufuli amefanya mazungumzo na Rais Idriss Deby Itno Ikulu Jijini Dar es Salaam.

clouds stream