Sunday 8 October 2017

ACT Watishia Kutinga Mahakamani Kupinga Uteuzi Wa JPM



Chama cha ACT-Wazalendo.

Chama cha ACT Wazalendo leo kimeibuka na kusikitishwa kwake na uteuzi wa Katibu wa Bunge mpya uliofanywa na Rais, Dkt.
John Pombe Magufuli mapema jana.
Rais Magufuli amemteua, Steven Kagaigai kuwa Katibu wa Bunge na aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo, Thomas Kashililah
atapangiwa kazi nyingine.
Kupitia taarifa yake iliyosainiwa na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano, Ado Shaibu, ACT imesema Rais ameamua kuyaweka
pembeni matakwa ya sheria yanayoongoza mchakato wa uteuzi wa Katibu wa Bunge na kuamua kujichagulia apendavyo.
“Kutokana na unyeti wa nafasi ya Katibu wa Bunge, na kwa minajili ya kuweka ‘check and balance’ pamoja na kulinda uhuru wa Bunge, kwenye mchakato wa uteuzi wa nafasi husika, sheria imeweka utaratibu wa kufuatwa kwenye uteuzi wa Katibu wa Bunge,”imesema taarifa hiyo.
ACT wamedai kuwa, mbali na Rais kuwa na mamlaka ya kumteua Katibu wa Bunge kwa mujibu wa Ibara ya 87 ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano, anapaswa kuzingatia utaratibu uliowekwa na Sheria ya Utawala wa Bunge ya mwaka 2015.
Kwa mujibu wa kifungu cha 7(3) cha sheria hiyo, Rais atateua jina moja kutoka miongoni mwa majina matatu yaliyopendekezwa naTume ya Huduma za Bunge.
“Jambo hilo si la hiari bali ni sharti la lazima la sheria ambalo Rais analazimika kulifuata. Ndiyo maana kifungu husika kinasema,
‘The Commision shall recommend three names. (Tume ni lazima ipendekeze majina matatu)’,” imeongeza taarifa hiyo.
ACT imesema kwa mujibu wa taarifa ambazo chama hicho kinazo, hakuna kikao chochote cha wajumbe wa Tume ya Huduma za
Bunge kilichoketi na kupendekeza majina kwa Rais kwa ajili ya uteuzi wa Katibu wa Bunge.
Chama hicho kimesema uteuzi huo ni ushahidi wa wazi wa kudharauliwa mhimili wa Bunge na kuahidi kufikisha suala hilo
mahakamani kama Rais hatatengua uteuzi huo na kufuata utaratibu uliowekwa na sheria za nchi.
“Ni matumaini yetu kuwa Bunge na watu wote wanaopenda uhuru na uimara wa Bunge watasimama imara kuupinga uteuzi huu
ambao ni kinyume cha sheria,” amesema Shaibu katika taarifa hiyo.

clouds stream