Friday 13 October 2017

Marekani, Israel Zajitoa UNESCO






Marekani na Israel zimetangaza kujiondoa kutoka Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) kwa kilekilichodaiwa kuwa ni kubaguliwa kwa taifa la Israel.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesema kuwa itabuni ujumbe wa waangalizi kwenye shirika hilo lenye makao yake nchini Ufaransa kuchukua mahala pa uwakilishi wake.

Mkuu wa UNESCO, Irina Bokova, amesema amesikitishwa na uamuzi huo lakini hajashangazwa.
Tangu wakati wa kampeni zake, Rais Trump alikuwa akitoa matamshi ya kuubeza Umoja wa Mataifa na pia kulalamika kwamba Marekani ndio inayochangia fedha nyingi zaidi, hivyo kudai kwamba atapunguza mchango wake.

Mwaka 2011, Marekani ilifuta bajeti yake kwa UNESCO ili kupinga hatua yake kuwapa Wapalestina uanachama kamili.

Marekani hutoa asilimia 22 ya bajeti ya kawaida ya Umoja wa Mataifa na asilimia 28 kwa shughuli za amani za Umoja wa Mataifa.

Unesco iko katika mikakati ya kumteua kiongozi mpya huku mawaziri wa zamani wa Qatari na Ufaransa, Hamad bin Abdulaziz alKawari na Audrey Azoulay wakiwa mstari wa mbele katika ushindani.

clouds stream