Sunday 1 October 2017

Mbunge Chadema Aweka Hadharani Ushahidi Madiwani Walivyonunuliwa





Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari ameweka hadharani ushahidi wa rushwa waliyopewa waliokuwa
madiwani wa Chadema ambao wamejiuzulu kwa madai ya kumuunga mkono Rais Magufuli na kuhama chama hicho.
Nassari ambaye aliambatana na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema walitoa ushahidi huo mbele ya waandishi wa habari na kueleza kuwa wataukabidhi katika mamlaka husika leo ikiwemo Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) na katika
taasisi nyingine.
Katika ushahidi wa video uliorekodiwa viongozi kadhaa wakiwemo Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Alexander Mnyeti pamoja
Mkurugenzi Mtendaji wa (H) Meru Christopher Kazeri wamesikika wakiwashawishi madiwani kuhama na baadhi waliahidiwa
wangelipwa posho za vikao vyao vilivyobaki hadi 2020 na kukamilishwa miradi yao.
Miongoni mwa makubaliano hayo ni kuwa wapewe fedha na kupata ajira na kukamilishwa miradi yote ya maendeleo waliyoahidi ikiwa ni pamoja na wengine kubadilishiwa makazi pamoja na diwani mmoja kusaidiwa gharama za kufanikisha harusi.
“Tutafikisha ushahidi huu katika ofisi za TAKUKURU Dar es Salaam kwa ajili ya kuukabidhi kwa Mkurugenzi Valentino Mlowola,”amesema.
Hatahivyo wakati Nassari akitoa ushahidi huo hadharani, madiwani 10 wa Chadema tayari wameshapokelewa ndani ya CCM huku wengine wakiwa wamepinga vikali kuhama chama hicho kwa sababu ya rushwa.
Aidha Nassari amesema ameamua kutoa ushahidi huo sasa kwa sababu alikuwa akiendelea kukusanya ushahidi wa kutosha.
“Mimi sina tatizo kwa mtu mmoja kuhama chama kwa utashi wake, ila kuhama kwa njia za kushawishiwa kwa rushwa ndiyo kitukibaya sana na ninataka Rais Magufuli achukue hatua dhidi ya jambo hili ili asihusishwe na uovu huu,” ameongeza.

clouds stream