Monday 16 May 2016

Tutunze Mabasi Ya Mwendokasi Yatutunze-Jaffo

Tutunze Mabasi Ya Mwendokasi Yatutunze-Jaffo

Tarehe May 16, 2016Basi-Darts
Wananchi wametakiwa kutunza miundombinu ya mradi wa Mabasi yaendayo Haraka (DART) pamoja na mabasi yenyewe ili kuufanya mradi huo wa kipekee katika nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki kuwa endelevu.
Rai hiyo imetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI Seleman Jaffo, na kuongeza kuwa Tanzania itakuwa miongoni mwa nchi zenye maendeleo makubwa baada ya kukamilisha miradi mikubwa iliyo kwenye mpango ya utekelezwaji, ukiwemo ujenzi wa barabara za juu ‘fly over’ kwenye makutano ya Barabara za Nyerere na Mandela ambako harakati za ujenzi zimeanza.
Naibu Waziri huyo amesema maendeleo hayo yataenda sambamba na ukamilishaji wa awamu ya pili ya mradi wa DART utakaohamia Barabara ya Kilwa itakayowaunganisha wakazi wa Mbagala kabla ya mradi wa tatu utakaowahusu wakazi wa Gongo la Mboto.
Amewataka watendaji wa DART kuharakisha mfumo wa ulipaji wa nauli kwa kutumia kadi ili kuepuka upotevu wa mapato unaoweza kusababishwa na watu wasio waaminifu huku akiliagiza Jeshi la Polisi kuimarisha ulinzi kuanzia vituoni.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa UDART David Mgwassa amesema huduma ya mabasi hayo itaanza saa 11:00 alfajili hadi saa 6:00 usiku kwa kutumia mfumo wa tiketi ambazo zitapatikana katika kila kituo huku wakiendelea kukamilisha mfumo wa kadi uanaotarajiwa kuanza kutumika rasmi baada ya siku tano.

clouds stream