Thursday 26 May 2016

Makandarasi 4,572 Wafutiwa Leseni

Makandarasi 4,572 Wafutiwa Leseni

May 27, 2016

V 1

Kaimu Msajili wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Rhoben Nkhori.

Bodi ya Usajili wa Makandarasi imefuta usajili wa jumla ya makandarasi 4,572 kwa kushindwa kutimiza matakwa ya Sheria ya Usajili wa Makandarasi ya mwaka 1997.

Kaimu Msajili wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Rhoben Nkhori amebainisha hayo wakati wa Mkutano wa Mashauriano wa CRB uliofanyika jijini Dar es Salaam na kufunguliwa na Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Nkhori amesema kuwa katika jukumu la kuratibu mwenendo wa kazi za makandarasi, Bodi ilikagua miradi 2735. Katika miradi hiyo iliyokaguliwa, miradi 1873 sawa na asilimia 68.5 haikuwa na kasoro.

Ameongeza kuwa miradi mingine ilikuwa na kasoro za kutofanywa na makandarasi waliosajiliwa, kutozingatia usalama wa wafanyakazi, kutokuwa na bango wala uzio na miradi kutosajiliwa. Kwa mujibu wa Bw. Nkhori miradi yote iliyopatikana na upungufu wahusika walichukuliwa hatua mbali mbali kwa mujibu wa sheria.

“Kwa mwaka jana, Bodi ilisajili miradi 3,172 yenye thamani ya shilingi trilioni4.23. Katika miradi hii asilimia 44.4 ilifanywa na Makandarasi wazawa na asilimia 55.6 ilifanywa na makandarasi wa kigeni,” amesema.

Licha ya mafanikio hayo CRD ilikumbana changamoto kadhaa ikiwemo kuwasilisha nyaraka za kugushi wakati wa usajili hususani kadi za magari na mitambo, vyeti vya wataalam, kutumia majina ya makandarasi kwa udanganyifu kwa kuuza vibao, waendelezaji kutotoa taarifa sahihi za umiliki kwa Bodi na baadhi ya makandarasi kushindwa kuwalipa wafanyakazi na vifaa vya ujenzi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi, Bi Consolata Ngimbwa amemwomba Mhe. Rais John Pombe Magufuli kuwapa kipaumbele Makandarasi wa humu nchini ili kuwawezesha kiuchumi. “Mhe. Rais tunaomba utupe kipaumbele kwani sisi tukipata hiyo miradi tutawekeza hapa nchi na kuongeza soko la ajira,”alisema Bi Ngimbwa.

Rais Magufuli amesema serikali yake itawapa kipaumbele makandarasi wazawa lakini akawataka wajipange na kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia maadili ikiwemo kujiepusha na vitendo vya rushwa.

clouds stream