Friday 14 July 2017

DCI AGEUKIA SAKATA LA MCHELE WA PLASTIKI , ATOA ONYO KALI


Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Boaz.
Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Boaz.
IMG-20170426-WA0006

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Boaz, ametoa onyo kali kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii kwa lengo la upotoshaji na kuliagiza Jeshi la Polisi kuanza mara moja kuwashughuliakia na kuwachukulia hatua za kisheria watu wenye tabia hiyo.

DCI Boaz ametoa onyo hilo baada ya hivi karibuni kuzuka taarifa katika mitandao ya kijamii kwa njia ya video ikionyesha uwepo wa mchele wa plastiki nchini.

Boaz amekanusha uwepo wa mchele huo wa plastiki na kuahidi kumsaka kwa udi na uvumba mtu aliyerekodi video hiyo ili asaidie kutoa taarifa zaidi.

Amewaomba wananchi kutumia vizuri mitandao ya kijamii na kujiepusha kusambaza taarifa zisizokuwa na ukweli, kwani ni hatari na husababisha madhara makubwa katika jamii.

”Kabla ya kusambaza taarifa kwanza uwe na uhakika wa vyanzo vyako, wahusika wanaweza kuingia kwenye matatizo yasiyokuwa ya msingi,” amesema DCI Boaz.

Aidha tayari Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ametaarifiwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kuwa hakuna mchele wa aina hiyo nchini.

Naye Waziri Ummy amewasisitizia watanzania kuwa makini na matumizi ya mitandao ya kijamii na kuepuka upotoshaji.

clouds stream