Sunday 16 July 2017

Lowassa, Kenyatta Wawaomba Wakenya Kuvumiliana

Mwanasiasa Edward Lowassa.

Mwanasiasa Edward Lowassa.
IMG-20170426-WA0006

Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amewataka Wakenya kuvumiliana wakati huu ambapo taifa hilo linakaribia uchaguzi.

Akizungumza nchini Kenya katika mazishi ya aliyekuwa waziri wa usalama nchini humo marehemu Joseph Nkaiserry, Lowassa amesema kuwa Kenya inapaswa kujifunza kutoka kwa machafuko ya uchaguzi ya mwaka 2007.

Matamshi yake yaliungwa mkono na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta aliyewataka wafuasi wake na wale wa kiongozi wa upinzani Raila Odinga kuvumiliana.

Uhuru amesema kuwa hakuna haja ya kupakana matope na matusi kwakuwa matusi hayasaidii.

“Sisi sote ni Wakenya, hatuna taifa jingine la kujenga baada ya uchaguzi, tunaomba amani, amani amani,” amesisitiza Rais Uhuru Kenyatta.

kenyatta

Rais wa nchi ya Kenya, Uhuru Kenyatta

Matamshi ya Uhuru na Lowassa yanakuja wakati ambapo wafuasi wa upinzani na wale wanaounga mkono serikali wamekuwa wakiwazomea viongozi wanaotoka pande pinzani katika mikutano ya kampeni na hata kusababisha mikutano hiyo kusitishwa.

Lowassa amesema kuwa Kenya ni tegemeo la kiuchumi katika mataifa ya Afrika Mashariki hivyo basi inafaa kuwa mfano kwa kuhakikisha kuwa taifa hili halijiingizi tena katika jinamizi la machafuko yalioonekana miaka 10 iliyopita.

“Ombeni sana msirudi katika mapigano yaliyotokea mwaka 2007, Kenya iko mbele kushinda taifa lolote lile Afrika Mashariki na tunataka muendelee kusonga mbele,” amesema Lowassa ambaye alikuwa Mgombea Urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kwa tiketi ya Chadema.

clouds stream