Friday 14 July 2017

Diallo Afunguka TRA Kufunga Kampuni Yake Na Akaunti Zake

Mmiliki wa Sahara Media, Anthony Diallo.
Mmiliki wa Sahara Media, Anthony Diallo.
IMG-20170426-WA0006

Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Sahara Media Group, Anthony Diallo amekiri kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imefungia akaunti ya kampuni yake na kudai kuwa masuala hayo yatamalizika bila rabsha yoyote.

Amesema kuwa ni akaunti moja tu iliyofungiwa na kwamba anaamini kuwa baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na mamlaka hiyo, watafikia muafaka ili biashara ziendelee kama kawaida.

“Tutalimaliza hakuna kitakachoenda mrama,” amesisitiza Diallo ambaye amewahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini ikiwamo nafasi ya Waziri wa Maliasili na Utalii na Naibu Waziri wa Maji, Maendeleo ya Mifugo katika Awamu ya Nne chini ya Rais MstaafuJakaya Kikwete.

Amesema deni la TRA linatokana na kodi iliyopatikana baada ya ukaguzi wa vitabu kwa miaka mitatu.

“Ni ukaguzi wa kawaida ambao hufanyika kama taratibu. Sasa kwa sababu ya kuhamisha matangazo yetu kutoka analojia kwenda digitali ilibidi tukope benki, ujenzi na kumaliza mradi imechukua miaka mitatu.

Wakati wote tumekuwa tukilipa riba benki na zinazobaki toka mauzo ya matangazo tunalipa mishahara, umeme na malipo ya kodi za kawaida,” amesema Diallo.

“Ni mambo ya kawaida ila wamefanya hatua za kutuaibisha tu. Kampuni yetu ya ving’amuzi na ni ya Kitanzania na mapato yote yanaingia nchini wakati kampuni nyingine kubwa zote ni za kigeni kutoka China, Afrika Kusini, Mauritius na Kenya. Ukweli sisi tunahitaji kusaidia nchi kiuchumi na kutuharibia ni hasara kwa nchi,” amefunguka Diallo.

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeunga ofisi za Sahara Media ambazo ni vituo vya redio vya KISS FM, RFA na cha luninga cha Star TV na kudaiwa kukamata akaunti za kampuni hiyo kwa kushindwa kulipa deni la Shilingi bilioni 4 kama kodi iliyopaswa kulipwa na kampuni hiyo.

Taarifa zilizosambaa kupitia mitandao ya kijamii zilieleza kuwa akaunti zote za kampuni hiyo zimefungiwa mpaka pale watakapolipa deni hilo, lakini kampuni hiyo imetoa ufafanuzi na kudai kuwa ni akaunti moja tu iliyofungwa.

clouds stream