Tarehe September 22, 2016
Edward Lowassa
Aliyekuwa Mgombea Urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Edward Lowassa, ameelezea wasiwasi wake juu ya dhamira ya Serikali kwa upinzani kutokana na migogoro inayozidi kukua baina ya viongozi wa Mkoa wa Arusha na Chadema na kudai kuwa ni mpango mahususi wa Serikali kutaka kukatisha tama vyama vya upinzani.
Amesema mipango hiyo ya Serikali inalenga kuvikatisha tama vyama vya upinzani ili visitekeleze majukumu yake kwa wananchi.
Lowassa ambaye pia alikuwa Waziri Mkuu kabla ya kuhamia Chadema Julai, mwaka jana, amesema hayo akiwa nyumbani kwake Monduli baada ya kuulizwa kuhusu hali ya kisiasa inayoendelea Mkoani Arusha kati ya viongozi wa Serikali na Chadema ambayo ndiyo inayoongoza Halmashauri ya Jiji la Arusha.
“Kinachoendelea Arusha ni mkakati wa Serikali wa kutaka kukandamiza upinzani na kuvikatisha tamaa vyama vya upinzani ili visitekeleze majukumu yake na mwisho wasifanikiwe katika mambo yao,” amesema Lowassa.