Tarehe September 22, 2016
Madereva wa Tanzania waliokuwa wametekwa na askari wa Kikundi cha Uasi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) wamesema kuwa njaa ya watekaji nduiyo iliowaokoa kirahisi kupitia majeshi ya nchi hiyo.
Mmoja kati ya madereva hao kumi amesema hayo mara tu baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JNIA) huku kukiwa na vilio, machozi na furaha kwa ndugu, jamaa na marafiki waliofika kuwalaki na kuwapokea madereva hao.
Dereva huyo, Athumani Fadhili amesema baada ya kuishiwa chakula watekaji hao walilazimika kumtuma mmoja wao ili aende kutafuta chakula maeneo ya Mjini na ndipo alipogundulika na majeshi ya Congo ambayo yaliamua kumfatilia kwa karibu akiwa anarudi ndipo walipoweza kutukomboa.
“Waliorodhesha majina yetu kwa kutumia pasipoti zetu, kutuhoji taarifa kuhusiana na familia zetu, mabosi wetu, kama tumeoa au la na kuziandika. Walitutembeza maeneo ya porini na kila walipokuwa wakihisi majeshi yanawakaribia walikuwa wakituhamisha hadi siku tuliyokombolewa,” amesema Fadhili huku akibubujikwa na machozi.