Monday, 5 September 2016

Kenyatta Adai Hakuna Mvutano Wa Kiuchumi Kati Ya Tanzania Na Kenya.

Tarehe September 5, 2016
1V 1

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amekanusha ripoti za vyombo vya habari kwamba kuna mvutano wa kiuchumi baina ya Kenya na Tanzania.

Kenyatta ameyasema hayo Mjini Mombasa wakati wa ufunguzi wa gati la makontena katika bandari ya Mombasa na kupuuzia maneno kwamba kuna mvutano wowote wa kiuchumi baina ya nchi hizo na badala yake akasema kuwa nchi hizo zinasaidiana.

Amesema anaona kwenye vyombo vya habari kwamba kuna mgogoro baina yetu, lakini nataka kusema wazi wazi kwamba Kenya na Tanzania hazina mgogoro wowote baina yao.

Kenyatta amesema uchumi wa nchi hizo mbili umefungana kwa miaka mingi na ni kwa ajili ya faida ya watu wa nchi hizo mbili.

Amesema kufunguliwa kwa njia inayojulikana kama “Northern Frontier” ambayo itaunganisha bandari ya Mombasa kupitia mkoa wa Kilimanjaro, Tanzania, hadi Bujumbura, Burundi itafupisha urefu wa kutoka Bujumbura hadi Mombasa kwa kilomita 300 nzima.

“Afrika Mashariki haiko katika mashindano ya wenyewe kwa wenyewe na kuongeza kuwa Afrika Mashariki inashindana na dunia. Tunataka kujadiliana ili pale penye mapungufu tuparekebishe ili tutumie nguvu zetu kukua, kuendeleza na kuinua uchumi wetu,” amesema.

Kutokuwepo kwa Rais John Magufuli wa Tanzania katika Mkutano wa hivi karibuni wa kimataifa na Tokyo mjini Nairobi kulizusha uvumi kuhusu uhusiano wa nchi za eneo hilo.

Kiongozi huyo wa Tanzania ametembelea Uganda na Rwanda tu tangu achukue madaraka Oktoba mwaka jana ukilinganisha na Rais aliyemtangulia Jakaya Kikwete ambaye alikuwa akisafiri sana nchi za nje.

Rais Magufuli pia hakuhudhuria mikutano karibu mitano ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na mkutano wa shirika la biashara duniani na mikutano mikuu ya AU Mjini, Addis Ababa na ule wa Kigali Rwanda hivi karibuni.

clouds stream