Tarehe September 24, 2016
Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam Alhad Mussa Salum akionyesha gazeti lilitoa taarifa ya uongo.
Viongozi wa Dini nchini, wamesema sio kweli Rais, Dkt. John Pombe Magufuli amekataa kuzungumza wala kuwapuuza kukutana na viongozi hao ambao wamemuomba kukutana naye, tofauti na inavyoenezwa na baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam Alhad Mussa Salum, amesema hayo Jijini Dar es Salaam kufuatia taarifa zilizochapishwa na gazeti la Tanzania Daima la Septemba 21 ISSN 0856 9762 toleo na. 4310 na kudai kuwa sio za kweli.
“Taarifa hizo sio za kweli, taarifa hizo zimelenga kumgombanisha Rais na Viongozi wa Dini na watanzania kwa ujumla na hilo halitafanikiwa,” amesema Sheikh Salum.
Aidha Viongozi hao wamesema uamuzi wao wa kumuomba Rais kuonana naye, haujatokana na kuagizwa na UKAWA, bali umetokana na maono waliyopewa na Mwenyezi Mungu.
Amefafanua kuwa Rais Magufuli anawaheshimu sana Viongozi wa Dini na mara zote amekua akiwaomba wamuombee na kusema leo ni siku ya tano tangu wamuandikie barua ya kumuomba kukutana naye na wanaimani Rais atakutana na Viongozi hao.
Ameeleza kuwa Barua hiyo imeandikwa Septemba 19 na kupelekwa siku hiyo hiyo Ikulu, ikiwa imesainiwa na Katibu Mkuu wa Bakwata, Katibu Mkuu wa CCT na Katibu Mkuu wa TEC.
“Naomba watanzania wasisikilize maneno hayo kwasababu hayana nia njema kwa Taifa letu, naamini Mheshimiwa Rais tutaonana nae na tutaongelea mustakbali wa nchi katika mambo mbalimbali,” ameongeza Sheikh Salum.
Akizungumzia utendaji wa Serikali ya Rais Magufuli, Sheikh Salum amesema Rais amerejesha nidhamu Serikalini, ukusanyaji mapato umeimarika na pia pengo kati ya wasionacho na walionacho linaanza kupungua.