Thursday, 1 September 2016

Mkapa Ataka Mageuzi Makubwa Sekta Ya Uwekezaji

Tarehe September 1, 2016
Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa.V 1
Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa.

Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, amezitaka nchi za Africa Mashariki kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya uwekezaji ili kuweza kuleta maendeleo barani humu.

Mkapa amesema hayo wakati akizungumza kwenye hafla ya Taasisi ya Mazingira ya Uwekezaji Afrika (ICF), ya kusherehekea miradi ipatayo 73 ya mageuzi ambayo imelenga kuifanya Afrika kuwa sehemu bora ya kufanyia biashara.

Mkapa ambaye pia ni Mwenyekiti Mweza wa Bodi ya ICF, iliyoudwa kwa lengo la kuthibitisha uwepo wa mageuzi ya haraka katika sekta ya uwekezaji ameshauri matumizi ya fedha kidogo kidogo kwa lengo la kuleta matokeo makubwa katika sekta binafsi, serikali pamoja na nchi kwa ujumla.

“Imefikia kipindi kwa nchi za Afrika kufuata mfumo huu wa ICF ili kuweza kuleta mageuzi makubwa ya uwekezaji katika sekta mbalimbali zikiwemo za kiserikali pamoja na binafsi na uwepo wa ongezeko la wajasiriamali, ” amesema Mkapa.

 Amesema miradi mingi iliyoweza kutekelezwa kati mwaka 2007 na 2016 imesaidia kusajiliwa kwa miradi mingine mingi, kulipa kodi zao kwa urahisi, kupitisha mizigo kwa mfumo wa forodha kwa haraka na urahisi pamoja na kusuluhisha migogoro ya kibiashara.

Mkapa amesema, mfumo wa ICF umeweza kufanya kazi barani Afrika katika nchi zipatazo 21, kuweka mfumo mmoja wa kielektroniki kwa lengo la kurahisisha uondoshwaji wa mizigo na kuweka mifumo ya mtandao ya ulipaji kodi.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya ICF, Neville Isdell ameyataja maeneo maalum ya mafanikio, ikiwa ni pamoja na kuundwa kwa mahakama tisa za kibiashara na nne za usuluhishi kwa lengo la kusuluhisha migogo ya kibiashara kwa haraka na uwazi.

Isdell amesema, mfumo wa ICF umeweza kusaidia badhi ya nchi kuweza kuwa na mfumo wa kielektroniki wa uuzaji wa bidhaa, kukuza uwezo wa serikali kushirikiana na sekta binafsi kwa kupitia mpango wa ushirikiano kati ya sekta za umma na sekta binafsi.

clouds stream