Tarehe September 21, 2016
Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola amemtaka mchezaji wa klabu hiyo, Yaya Toure kuomba radhi kutokana na maneno mabovu aliyoyasema wakala wake vinginevyo hataichezea timu hiyo.
Toure, 33, ameichezea City mchezo mmoja tu tangu msimu huu uanze na ameachwa rasmi katika kikosi cha City kitakachoshiriki michuano ya Klabu Bingwa Ulaya.
Wakala wake, Dimitri Seluk alikaririwa akisema kuwa kiungo huyo ‘amedhalilishwa’ na Guardiola atapaswa kumuomba radhi kama City haitachukua ubingwa.
Amesema ni lazima Toure aombe msamaha na kama hataki hatacheza kamwe.
Kocha huyo vilevile anataka kuombwa radhi na wakala huyo Seluk na kukiri kuwa ulikuwa uamuzi mgumu sana kumuacha Toure katika kikosi cha ligi ya mabingwa ulaya.
Guardiola ameyasema hayo muda mfupi tu baada ya Toure ambaye pia ni kiungo wa Kimataifa wa Ivory Coast kutangaza kustaafu kuichezea timu ya Taifa ya Ivory Coast
Akiwa ameanza kuichezea timu ya taifa mwaka 2004, Toure ameshinda jumla ya mechi 113 akiwa na timu ya taifa, ikiwa ni pamoja na Kombe la Mataifa ya Afrika, mwaka 2015.
“Baada ya miaka 14 ya kiwango cha juu, nina uhakika kuwa huu ni muda muafaka wa mimi kufanya hivyo,” amesema Toure katika taarifa aliyoitoa huku akikiri kuwa kuandika taarifa hiyo pengine ni moja ya wakati mgumu sana katika maisha yake.