Tarehe September 7, 2016
Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka.
Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umesema hakuna baya lolote lililotamkwa na Rais, Dkt. John Pombe Magufuli katika mikutano yake ya Unguja na Pemba isipokuwa amezika upotoshaji wa siasa uchwara, kusafisha upepo mchafu na kufumba vinywa vya wanasiasa wakorofi na wazushi.
Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka amesema shutuma anazotupiwa Rais Magufuli ikidaiwa na baadhi ya wanasiasa kwamba alilenga kuamsha joto la mtafaruku wa kisiasa visiwani humo hazina tija.
Amesema hotuba ya Rais Dkt. Magufuli imezima siasa za uzushi dhidi ya viongozi wanaowadanganya wafuasi wao kwamba utafanyika Uchaguzi Mkuu mwingine kabla ya mwaka 2020 na Rais Ali Mohamed Shein ataondoka madarakani ili kumpisha Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad na ilikuwa yenye mashiko na maudhui ya makatazo, maonyo, maelezo na wosia uliojiegemeza katika kudumisha amani nchini.
“Kuhubiri amani ni dhamana yake kiutawala, kuwaonya wananchi wanaokata mikarafuu, kutoboa mitumbwi, kufyeka mazao mashambani na wengine kukataa kuwauzia bidhaa wenzao halikuwa kosa na si jambo baya kama inavyoelezwa na wazushi wa kisiasa,” alisema Shaka.
“Iweje baniani mbaya kiatu chake dawa, unajigamba humtambui Rais aliyeshinda na kuunda serikali ila unadoea fedha zinazokusanywa na serikali usioitambua ili usaidiwe na kulipwa marupurupu. UVCCM inaunga mkono SMZ kumnyima stahili zote hadi atakaipomtambua Rais,” amefunguka Shaka.
Kaimu Katibu Mkuu huyo amedai kuwa wakati wa utawala wa Dkt. Salmin Amour Juma, Maalim Seif aliposema hamtambui kama mshindi halali hakuwa akilipwa chochote, Rais mstaafu Amani Abeid Karume hakumlipa kitu hadi alipojipeleka Ikulu Novemba 5, 2009 akatangaza kuitambua serikali yake.
Ametoa wito kwa Wazanzibari kwa nguvu zote kupinga siasa chafu au zenye lengo la kuwagawa, kuwatenganisha au kuwahasimisha badala yake watambue umuhimu wa kuendeleza umoja, amani na maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Hivi karibuni akiwa ziarani Visiwani Zanzibar, Rais Magufuli alimtaka Rais wa Zanzibar kupunguza upole na kumshangaa kwa kuendelea kusaini mambo ya Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif ilhali alimpa mkono wake akaukataa.
Hotuba hiyo ilizusha minong’ono kadhaa hadi kupelekea CUF kuja na tamko rasmi wakilaani vikali hotuba ya Rais Magufuli visiwani humo.