Tarehe September 28, 2016
Baraza Kuu la Chama cha Wananchi CUF leo limemtimua uanachama alikyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba.
Uamuzi huo umefikiwa leo katika kikao kilichoongozwa na Mbunge wa Tandahimba, Katani Ahmed Katani baada ya kuungwa mkono na wajumbe wote 43 waliohudhuria kikao hicho.
Mashtaka dhidi ya Lipumba alirejea katika nafasi yake ya Uenyekiti kufuatia barua kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, yaliandaliwa na Sekretarieti ya CUF ikimtuhumu kufanya vurugu, kuharibu mali za chama na kudharau barua ya wito wa chama hicho iliyomtaka kwenda kujitetea.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Lipumba akiongozana na wafuasi wake chini ya ulinzi wa polisi walidaiwa kuvunja geti na milango ya ofisi ya chama hicho katika Makao Makuu Buguruni, Jijini Dar es Salaam na kuingia katika ofisi hizo.
Aidha, Baraza hilo limeukataa ushauri na mwongozo wa Msajili wa Vyama vya siasa alioutoa kwa chama kwa sababu umekiuka matakwa ya Sheria ya Vyama Vya Siasa ya Tanzania, hauna mantiki na mashiko ya kisheria na unakiuka matakwa ya katiba ya CUF.
Baraza hilo pia limesema Kamati ya Uongozi liliyoiunda ndiyo inayotambulika kikatiba hadi hapo atakapochaguliwa Mwenyekiti mpya wa CUF.