Thursday, 15 September 2016

JK Aunga Mkono JPM Kusitisha Safari Ya Zambia Kushiriki Maafa Ya Tetemeko.

Tarehe September 15, 2016
magufuli_

Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Kikwete ameunga mkono uamuzi wa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli wa kuahirisha safari ya kwenda nje ya nchi ili kuweza kushiriki katika maafa ya tetemeko la ardhi lililotokea hivi karibuni Mkoani Kagera.

Katika salamu za pole alizomtumia Rais Magufuli na wahanga wote wa tetemeko hilo wakati wa hafla ya makabidhiano ya nyumba 22 za watumishi wa afya zilizojengwa na Taasisi ya Mkapa Mkoani Pwani iliyofanyika Kituo cha Afya Msoga, Chalinze, Kikwete amesema uamuzi huo ni wa busara sana kwa kuwa Serikali inatakiwa kufanya juhudi za makusudi kushughulikia tatizo hilo.

Amesema misaada ya haraka na dharura inahitajika ili waathirika waendelee kupata huduma zote muhimu hasa za kibinadamu.

“Ndugu zangu pamoja na kuwa leo hii tunakabidhiana nyumba 22 za watumishi wa afya Mkoani kwetu, naomba tusimame tuwakumbuke wenzetu waliopoteza maisha katika tetemeko la ardhi huko Bukoba na pia natumia fursa hii kutoa pole kwa waathirika wote na Rais, Dkt. John Magufuli,” amesema JK.

Ameongeza kuwa Rais Magufuli amefanya uamuzi wa busara sana kuahirisha safari yake ili kushiriki katika maafa haya.

clouds stream