Tarehe September 22, 2016
Serikali imesema inakusudia kuendesha kampeni maalum ya kupima matumizi ya vilevi kwa madereva wanaosafirisha abiria na mizigo ikiwa ni hatua ya kukabiliana na tatizo la ajali za barabarani nchini.
Hayo yamesemwa Jijini Dar es Salaam na Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Samwel Manyele alipokuwa akifungua mafunzo ya siku mbili kwa wadau wa kemikali juu ya matumizi salama ya kemikali nchini. Profesa Manyele alisema utaratibu wa kuwapima madereva hao utaanza hivi karibuni na utawezesha kupunguza tatizo la ajali barabarani na kuvitaka vyombo vya ulinzi na usalama kutoa ushirikiano katika zoezi hilo.
“Madereva wote wanaosafirisha mizigo na abiria watatakiwa kupita kwenye kipimo ambacho kitaonyesha kama madereva hao wanatumia vilevi, hali hiyo itasaidia kutatua tatizo la ajali za barabarani nchini,” amesema Manyele.
Profesa Manyele amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kutoa uwezo na uelewa kwa wahusika hasa wasimamizi wa shughuli za kemikali na matumizi salama juu ya kukabiliana na matukio au ajali za kemikali pale yanapotokea.