Tarehe September 19, 2016
Mji wa Kigoma kupitia Manispaa zake unatarajia kuwa Mji mkuu wa Mawese barani Afrika ifikapo 2020 kutokana na mipango mbalimbali ya kuzalisha na kuongeza thamani ya zao la mchikichi na mafuta ya mawese.
Hayo yamesemwa na Meya wa KigomaUjiji, Hussein Ruhava Juma wakati akitoa taarifa kuhusu Mpango wa Ushiriki na Uwajibikaji Serikalini (OGP) ambapo amesema kuwa mji wa Kigoma umechaguliwa kushiriki katika mpango huo unaoshirikisha miji 15 duniani kote.
“Kama mnavyojua mawese ni zao kuu la biashara kwa wakulima wa mkoa wa Kigoma lakini kwa kipindi kirefu manufaa ya mawese hajaonekana kwa wakulima kwa sababu ya kukosekana kwa soko la uhakika, uhaba wa viwanda vya kuongeza thamani pamoja na kukosekana kwa mbini bora za ukulima wa kisasa” alisema Mhe. Juma.
“Lakini kwa sasa manispaa ya KigomaUjiji imejipanga vyema kuhakikisha inapanda michikichi milioni 3 kuzunguka mji mzima kuanzia mwakani ili itakapofika mwaka 2020 mji wetu uweze kuvuna mafuta ya kutosha ili kuweza kuwa mji wa mawese barani Afrika” aliongeza.
Aidha Meya huyo wa Manispaa ya KigomaUjiji alisema kuwa mji wa Kigoma unatarajia kuvuna mafuta ya kutosha kwa miaka 25 mfululizo ambapo mafuta hayo yatakayovunwa yatakuwa na thamani ya dola 83 za kimarekani sawa na bilioni 170 za kitanzania kutokana na idadi ya miti ya michikichi itakayopandwa mwakani.
Pia Meya wa Manispaa ya KigomaUjiji amewataka wafanyabiashara wenye viwanda vya kuongeza thamani kuwekeza katika mji wa Kigoma kutokana na uzalishaji wa tani 80,000 za mawese ghafi zinazotarajiwa kuzalishwa kila mwaka kuanzia mwaka 2020.
Kuhusu mpango wa OGP Meya Juma amesema kuwa mji wa Kigoma umeweka viapaumbele sita viatakavyotumika kupima utendaji kazi wa manispaaa hiyo. Amevitaja viapumbele hivyo kuwa ni elimu, afya, maji, ardhi, uwazi katika bajeti na uwazi katika takwimu.