Thursday, 8 September 2016

Majaliwa Aridhishwa Na Kasi Ya Ujenzi Wa Makazi Yake Dodoma.

Tarehe September 8, 2016
1-2
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema uamuzi wa Serikali kuhamia Dodoma hautokani na shinikizo la kisiasa bali ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambao chimbuko lake ni agizo lililotolewa Oktoba Mosi, 1973 kwenye Mkutano Mkuu wa 16 wa chama cha TANU.
Majaliwa ameyasema hayo alipofanya ziara ya kukagua ujenzi wa makazi mapya ya Waziri Mkuu katika eneo la Mlimwa na kuagiza umalizike kwa wakati ili aweze kuhamia kama alivyoahidi.
Katika ziara hiyo aliyoifanya jana mchana (Jumatano, Septemba 7, 2016) Waziri Mkuu amesema ameridhishwa na namna kazi ya ujenzi inavyofanyika.
“Nimekuja kukagua makazi mapya na mahali pa kufanyia kazi. Kazi ya ujenzi inaendelea vizuri, nimejionea mwenyewe na naamini katika kipindi kifupi watakuwa wamekamilisha,” amesema.
Amedai kuwa kutokamilika kwa ujenzi huo hauwezi kukwamisha azma yake ya kuhamia Dodoma kwa sababu tayari inafahamika kuwa Makao Makuu ya Ofisi ya Waziri Mkuu yako Dodoma.
“Tangu wakati huo Serikali zote ziliendelea kufanya juhudi mbalimbali za kuandaa miundombinu na hata awamu ya nne ilisimamia kwa kiwango kikubwa uwekaji wa miundombinu hiyo,” amesema.
“Pia tukumbuke kauli ya Mheshimiwa Rais aliyotoa kwenye hotuba yake ya Julai 23, 2016 alipochaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa CCM, na akairudia tena Julai 25, kwenye maadhimisho ya kumbukumbu ya Mashujaa na mimi siku hiyo hiyo nikaweka msisitizo,” ameongeza.
Amesema uamuzi wa Serikali ya awamu ya tano wa kuhamia Dodoma unakuja baada ya kuridhishwa na ujenzi wa miundombinu na maeneo ya kutolea huduma za kijamii kwa wageni na wenyeji ikiwemo Hospitali ya Benjamini Mkapa iliyopo katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) yenye uwezo wa kutibu magonjwa makubwa kama ya moyo na figo.
Waziri Mkuu amesema tayari Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) ina mpango kamambe (master plan) na ina viwanja vya kutosha kujenga makazi na ofisi mbalimbali.32

clouds stream