Thursday, 15 September 2016

Mwanafunzi Kidato Cha Kwanza Ajifungua Bwenini.

Tarehe September 15, 2016
mimbapicha

Mwanafunzi wa kidato cha Kwanza, Helena Mpondo wa Shule ya Sekondari Mbalala, Manispaa ya Dodoma amejifungua mtoto akiwa ndani ya bweni huku kukiwa na utata wa namna alivyoondolewa shuleni hapo.

Helena anadaiwa kujifungua mtoto mwenye afya njema kwa usaidizi wa walimu na baadaye kuitiwa mganga wa zahanati ya jirani kwa ajili ya kumkata kitovu na msaada zaidi.

Ijumaa ya Septemba 2, mwaka huu majira ya saa tatu asubuhi mwanafunzi huyo alishikwa na uchungu akiwa peke yake bwenini, lakini matroni na mwalimu mwingine wa kike waliwahi kufika eneo hilo na kumsaidia kujifungua salama.

Mkuu wa Shule hiyo, Joram Mkwawa amesema siku ya tukio aliitwa na walimu wenzake na alipofika eneo la tukio alikuta mwanafunzi huyo ameshajifungua.

“Nilichofanya niliwaambia waende zahanati na nilituma pikipiki ya kumfuata mzazi wake ambaye alipofika nilimkabidhi mwanawe kwakuwa ni kosa kukaa na mtoto mwenye mimba,” amesema.

Mkwawa amesema inawezekana mwanafunzi huyo alijiunga shuleni hapo akiwa tayari na ujauzito lakini cha kushangaza ni kwa jinsi mimba hiyo haikuweza kujulikana hadi alipojifungua na kukanusha madai kuwa alimzuia mwanafunzi huyo kuondoka mchana hadi usiku uingie kwa minajili ya kuficha ukweli.

Naye mama Mzazi wa mwanafunzi huyo, Sara Mnyanyika amesema siku ya tukio alifuatwa na watu wawili wakiwa katika pikipiki na kumtaka aondoke nao haraka bila ya kumtaarifu chochote wakidai mwanangu ni mgonjwa mahututi.

“Nilipofika nilikuta mwanangu ameshapelekwa zahanati akiwa tayari na mtoto, kilichoniuma ni hawa watu kunibeba kwa nguvu bila ya kusema , nikaondoka bila hata ya nguo za mtoto na matokeo yake nikakuta mwanangu amemfunika mtoto na sweta la shule,” amesema Sara.

Mama huyo ameongeza kuwa baada ya hapo alikabidhiwa mwanae na mjukuu wake na kupewa sharti la kutoondoka hadi usiku uingie kwa madai kuwa uongozi wa shule haukutaka jambo hilo lifahamike kwa umma na hivyo kuzua sintofahamu ya nani anasema ukweli kati ya mama na mwalimu mkuu.

Katika taarifa aliyoitoa kwa Manispaa ya Dodoma, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Christina Mndeme alisema manispaa hiyo ilikuwa na wanafunzi 51 wenye mimba ambapo 45 kati yao walikuwa wa shule za sekondari na 6 shule za msingi.

clouds stream