Thursday 3 September 2015

Raia wa Burundi watimka, Tanzania yaelemewa na wakimbizi

Raia wa Burundi watimka, Tanzania yaelemewa na wakimbizi


Wakimbizi kutoka Burundi.
Idadi ya wakimbizi kutoka Burundi kuingia nchini Tanzania, inaendelea kuongezeka kila uchao. Umoja wa Mataifa umesema kuwa wakimbizi mia nne kutoka Burundi huvuka mpaka na kuingia Tanzania kila siku.
Kufikia sasa zaidi ya wakimbizi elfu tisini wamekimbilia nchi jirani ya Tanzania tangu mzozo wa kisiasa kuanza nchini Burundi, Aprili mwaka huu.
Kwa mujibu wa  Mkurugenzi wa Shirika na Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Joyce Mends-Cole amesema ziko sababu kadhaa zinazowafanya wananchi wengi wa Burundi wazidi kuikimbia nchi yao, kubwa likiwa hofu waliyo nayo juu ya usalama wao.
Mends-Cole amesema taarifa zinadai kuwa ingawa maeneo mengine ya Burundi yametulia bado hakujapatikana utulivu katika mji mkuu Bujumbura, na kumekuwepo na milipuko kadhaa ambayo inaweza kuwa chanzo cha hofu kwa wananchi wanaoikimbia nchi.
Mkurugenzi huyo wa UNHCR amesema pia kuwa shirika hilo limekuwa na mazungumzo na wenzao walioko Burundi kuona uwezekano wa kuwarejesha warundi nyumbani kwao lakini kwanza wanazingatia suala la usalama wa wale wanaokimbia maeneo yasiyo na usalama.
Aidha Mends-Cole amesema hivi sasa Kambi hiyo ya Nyarugusu inayowapokea wakimbizi hao imeelemewa na idadi kubwa ya watu na sasa Shirika lake la UNHCR limekuwa likifanya mazungumzo na Serikali ya Tanzania kuona kama wanaweza kuwaongezea eneo zaidi kwa ajili ya kufungua kambi nyingine za wakimbizi.
Umoja wa Mataifa unasema zaidi ya watu elfu tisini wameikimbia Burundi na kuingia Tanzania tangu kuanza kwa vurugu mwezi wanne mwaka huu.

clouds stream