Sunday 13 September 2015

TCRA yapiga marufuku vipindi vya ‘live’ uchaguzi mkuu 2015

TCRA yapiga marufuku vipindi vya ‘live’ uchaguzi mkuu 2015

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetangaza kupiga marufuku vipindi vya moja kwa moja  vinavyohusu uchaguzi mkuu kwenye vituo vya Televisheni.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mamlaka hiyo imebainisha kuwa kuanzia  tarehe 10 Septemba 2015, na katika kipindi chote cha kampeni za uchaguzi mkuu 2015, watu ambao sio wagombea wa udiwani, ubunge, urais, wasemaji rasmi wa vyama au watu wasioteuliwa na vyama vya siasa kama wawakilishi hawataruhusiwa kushiriki katika vipindi vya moja kwa moja (Live Programmes) vinavyohusu shughuli za uchaguzi vitakavyorushwa na vituo vya utangazaji hapa nchini.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa  utaratibu huu unazingatia Kanuni Za Huduma Za Utangazaji (Maudhui) (Utangazaji Wa Uchaguzi Wa Vyama Vya Siasa), 2015, Kanuni ya 4 (f), (h), (i),  5(b), (d), (e) and (f).
Mamlaka hiyo  imesema kuwa hatua hii inachukuliwa na Mamlaka ili kuweka utaratibu mzuri wa kufanya kampeni za uchaguzi ziwe za amani na utulivu huku ikiahidi kuchukua hatua kali dhidi kituo cha utangazaji kitakacho kwenda kinyume na utaratibu huu huo.
Hivi karibuni vimeibuka vipindi mbalimbali vinavyohusu uchaguzi mkuu hususani kwenye televisheni  ambavyo wachambuzi wake wamekuwa waki egemea upande mmoja wakitumia lugha ya kuudhi, kuchafuana baina ya wagombea mbalimbali wa urais ikiwemo wagombea wenye upinzani mkubwa sana hivisasa ambao ni Edward Lowassa na Dk.John Pombe Magufuli.

clouds stream