Friday 14 October 2016

Maadhimisho Ya Mwl. Nyerere Yafanyika Bila Uwepo Wa Familia Yake

Tarehe October 15, 2016
Mwalimu Nyerere akiwa na Nelson Mandela.V 2
Mwalimu Nyerere akiwa na Nelson Mandela.

Maadhimisho ya miaka 17 ya kumbukumbu ya kifo cha Mwalimu Julius Nyerere yalifanyika jana Mjini Bariadi Mkoani Simiyu bila kuwepo kwa familia ya mwasisi huyo wa Taifa.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka alisema Oktoba 5, mwaka huu Mama Maria Nyerere alikuwa miongoni mwa waalikwa katika sherehe hizo na mipango kwa ajili ya malazi yake na msafara ilikuwa imeandaliwa.

Katika mipango ya awali, mama Maria na msafara wake alipangiwa kufikia katika nyumba za halmashauri ya mji wa Bariadi zilizoko eneo la Nyamuata kabla ya kuhamishiwa katika hoteli mpya ya Sumayi.

Meneja wa Hoteli hiyo, Mabula Mapolu alithibitisha ugeni wa Mama Maria kupangiwa kufikia hotelini hapo lakini baadaye walipewa taarifa kuwa ugeni huo usingefika tena.

Mmoja wa watoto wa Mwalimu Nyerere, Madaraka Nyerere amesema yeye binafsi hakuona mualiko wa faamilia kuhudhuria sherehe hizo na kudai kuwa kama ulikuja basi huenda ulipokelewa na mwanafamilia mwingine kwasababu familia yao ni kubwa.

“Yawezekana mwaliko ulipokelewa na mmoja wa wanafamilia kutokana na familia yetu kuwa kubwa lakini aliyeupokea akapata hudhuru na kushindwa kufika kuhudhuria,” ameongeza Madaraka akielezea kutoonekana kwa familia hiyo katika maadhimisho hayo.

Amesisitiza kuwa hilo halimaanishi kuwa Serikali haikutoa mualiko kwa familia hiyo.

Familia hiyo jana ilishiriki ibada maalum katika Kanisa Katoliki Butiama ambayo pia ilihudhuriwa na viongozi kadhaa wa Serikali akiwemo Mkuu wa Mkoa huo, Dkt. Charles Mlingwa, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo aliyemuwakilisha Rais, Dkt. John Pombe Magufuli na Wakuu wa Wilaya wa Mkoa wa Mara.

clouds stream