Friday 14 October 2016

Serikali Yatangaza Vipaumbele Vipya Kupata Mkopo Chuo Kikuu

Tarehe October 15, 2016
Naibu Waziri wa Elimu Stella Manyanya.Naibu Waziri wa Elimu Stella Manyanya
V 2

Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, imebadilisha Vipaumbele katika fani za kusomea wanafunzi wa Vyuo Vikuu nchini kwa mwaka wa masomo 2016/2017.

Kwa mujibu wa taarifa yake Naibu Waziri wa Elimu Stella Manyanya amesema katika utekelezaji wa jukumu hili, Serikali imeandaa Sifa na Vigezo vya Utoaji Mikopo kila mwaka ili kuendana na malengo na matarajio yaliyopo katika mipango na mikakati ya kitaifa kama ilivyoainishwa katika Dira ya Taifa 2025, Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/17 ­2020/21), Sera ya Elimu na Mafunzo (2014) na Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Kwa kuzingatia mipango mikakati na sera hizo, pia Mwongozo wa utoaji mikopo kwa mwaka 2016/2017 katika mwaka wa masomo 2016/17, Serikali imetoa vigezo vitakavyozingatiwa katika utoaji mikopo kama ifuatavyo:

(i) Vipaumbele vya kitaifa vinayoendana na mpango wa maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na mafunzo ambayo yatazalisha watalaamu wanaokidhi mahitaji ya kitaifa katika fani za kipaumbele vifuatavyo:

· Fani za Sayansi za Tiba na Afya,

· Ualimu wa Sayansi na Hisabati,

· Uhandisi wa Viwanda, Kilimo, Mifugo, Mafuta na Gesi Asilia

· Sayansi Asilia na Mabadiliko ya Tabianchi

· Sayansi za Ardhi, Usanifu Majengo na Miundombinu

(ii) Uhitaji wa waombaji hususani wenye mahitaji maalum kama vile Ulemavu na Uyatima

(iii) Ufaulu wa waombaji katika maeneo ya vipaumbele na umahiri Kwa hivi sasa Bodi imekamilisha uchambuzi wa majina ya waombaji ambao wana sifa zilizoainishwa hapo juu na majina ya wanufaika wapya yametangazwa kuanzia jana tarehe 14 Oktoba, 2016.

Aidha, kuanzia mwaka huu wa masomo, wanufaika wote wa mikopo (wapya na wanaoendelea na masomo) watakopeshwa kulingana na uwezo wao (means tested) katika vipengele vyote vya mikopo.

clouds stream