Thursday 20 October 2016

Majambazi Mengine 6 Yauawa Dar

Tarehe October 20, 2016
majambaziV 2

Watu sita wanaosadikika kuwa majambazi hatari wameuawa katika majibizano ya risasi na Polisi katika eneo la Mbezi kwa Yusuf Makondeni katika Manispaa ya Kinondoni, Jijini Dar es Salaam.

Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Naibu Kamishna wa Polisi, Lucas Mkondya, amesema watuhumiwa hao waliuawa katika majibizano ya risasi na Kikosi Maalumu cha Kupambana na Ujambazi wa Kutumia Silaha.

Amesema walipata taarifa kutoka kwa raia mwema kuwa kuna kikundi cha watu wenye silaha, wamejipanga kufanya tukio la ujambazi kwa kutumia silaha kwa mfanyabiashara aliyekuwa akitoka Benki ya Diamond Trust Bank (DTB), tawi la Barabara ya Nyerere, ambaye angepita katika barabara hiyo kwenda mkoani Morogoro.

Amedai kuwa baada ya kupata taarifa hizo, polisi waliweka mtego na majambazi hao wakitumia gari aina ya Toyota Carina lenye namba za usajili T970 DGZ rangi ya fedha, walionekana wakilifukuza gari la mfanyabiashara huyo, kisha kulipita na kumsimamisha kwa nguvu.

“Majambazi wawili wakiwa na bastola walishuka katika gari hilo. Baada ya kugundua kuwa wameingia kwenye mtego wa polisi, walianza kufyatua risasi kwa askari wakitumia bastola na wenzao waliokuwa wamejaa kwenye gari yao walianza kushuka huku wakifyatua risasi kuelekea kwa askari,” amesema.

Ameongeza kuwa kutokana na hali hiyo askari walianza kujibu mashambulizi na kuwaua majambazi hao na baada ya upekuzi, zilipatikana bastola mbili, moja ya kijeshi aina ya Chinese ikiwa na risasi moja ndani ya kasha la risasi; na nyingine aina ya Browning ikiwa imefutwa namba zake na maganda sita ya risasi yaliyookotwa katika eneo la tukio.

Miili ya watuhumiwa hao imehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na upelelezi unaendelea ili kubaini mtandao mzima wa ujambazi.

clouds stream