Wednesday 13 May 2015

Azam yatoa ufafanuzi ujio wa Stewart Hall

Azam yatoa ufafanuzi ujio wa Stewart Hall


Kocha Stewart Hall anatajwa kujiunga na timu yake ya zamani Azam FC
Kocha Stewart Hall anatajwa kujiunga na timu yake ya zamani Azam FC
Baada ya taarifa kuzagaa juu ya uongozi wa Azam FC kumrudisha kocha wa zamani wa kikosi hicho Muingereza Stewart Hall, uongozi wa klabu hiyo umevunja ukimya kwa kuamua kutoa ufafanuzi juu ya tetesi hizo.
Mwenyekiti wa klabu hiyo Said Mohamed amesema, kwa sasa klabu yao ipo kwenye mchakato wa kutafuta kocha mwingine lakini kwenye orodha ya majina ya makocha wanaotaka kuwapa kibarua cha kukinoa kikosi chao ni pamoja na jina la Stewart Hall.
“Sisi sasa hivi tupo kwenye mchakato wa kutafuta mwalimu, kwahiyo majina yanakuwa mengi sana. Tuna majina karibu 12 mpaka sasa hivi, moja kati ya hayo ni la Stewart, lakini bado hatujakaa kikao cha kuchuja ili kupata jina moja”, amesema Mohamed.
Alipoulizwa kuhusu hatma ya George Nsimbe ‘Best’, Mohamed alisema, “George yeye alipewa kazi ya kuwa ‘care taker coach’ baada ya kuondoshwa Omog, sasa sio lazima apewe majukumu ya ukocha mkuu”, Mohamed alifafanua.
“Tukishapitisha jina tutalipeleka kwenye bodi ya timu, baada ya kila kitu kuwa kimekamilika, tutawaita waandishi wa habari na tutawaambia kila kitu ambacho kimeamuliwa”, alimaliza.
Hall alitimuliwa na uongozi wa Azam katikati ya msimu wa 2012-2013 na nafasi yake ikachukuliwa na kocha raia wa Cameroon Joseph Omog ambaye nae kibarua chake kiliota nyasi baada ya mabingwa hao wa zamani wa ligi kuu Tanzania bara kutupwa nje ya michuano ya vilabu bingwa Afrika na nafasi yake kuchukuliwa na Nsimbe ambaye alimalizia mechi zilizo salia kwenye ligi kuu huku akifanikiwa kuisaidia Azam kumaliza ligi ikiwa nafasi ya pili nyuma ya Yanga ambao ni mabingwa.

clouds stream