Monday 4 May 2015

Kopunovic: Simba ni timu bora Tanzania

Kopunovic: Simba ni timu bora Tanzania

Kocha mkuu wa Simba SC Goran Kopunovic
Kocha mkuu wa Simba SC Goran Kopunovic
Baada ya kufanikiwa kuwafunga Yanga ambao ni mabingwa wa ligi kuu msimu huu na waliokuwa mabingwa wa msimu uliopita Azam FC, kocha mkuu wa Simba SC Goran Kopunovic amesema, sasa swali la timu gani bora nchini limeshajibiwa.
“Niliiandaa vizuri timu yangu, Azam FC ni mabingwa na bado nawaona ni mabingwa, ni timu ngumu, nina furaha sana kwasababu nilikuwa na msongo wa mawazo, sio mimi tu, kila mtu ndani ya timu”, amesema Kopunovic
“Nina furaha sana, najivunia sana kuwa timu yangu ndio bora nchini Tanzania, tulimfunga Yanga, tumemfunga Azam, nadhani hakuna swali tena ni timu gani bora Tanzania”, Kopunovic alitamba.
‘Wekundu wa Msimbazi’ Simba wamefikisha pointi 44 katika nafasi ya tatu baada ya kucheza mechi 25, pointi moja nyuma ya Azam FC waliopo nafasi ya pili kufuatia kushuka dimbani mara 24.
Magoli ya Ibrahim Ajib na Ramadhani Singano ‘Messi’ yalitosha kuwapa Simba ushindi dhidi ya Azam FC katika mechi ya ligi kuu iliyopigwa jana kwenye uwanja wa Taifa. Goli pekee la Azam lilifungwa na kiungo Mudathir Yahya dakika ya 58.
Ili Simba wamalize ligi wakiwa nafasi ya pili, wanahitaji kushinda mechi yao ya mwisho Mei 9 dhidi ya JKT Ruvu uwanja wa Taifa, halafu Jumatano Azam wafungwe na Yanga na kutoa sare mechi ya mwisho dhidi ya Mgambo JKT.

clouds stream