Wednesday 13 May 2015

Pluijm aweka hadharani kikosi bora VPL 2014-2015

Pluijm aweka hadharani kikosi bora VPL 2014-2015


Kocha mkuu wa timu ya Yanga Hans van der Pluijm
Kocha mkuu wa timu ya Yanga Hans van der Pluijm
Msimu wa 2014-2015 wa ligi kuu ya soka Tanzania bara umemalizika mwishoni mwa juma lililopita (Mei 9 mwaka huu) na kushuhudia Yanga wakitangazwa mabingwa, Azam wakishika nafasi ya pili, Simba nafasi ya tatu, Mbeya City nafasi ya nne, huku Ruvu Shooting na Polisi Morogoro zikishuka daraja.
Kila kocha anapewa nafasi ya kutaja kikosi cha wachezaji 11 kutoka timu zote zilizoshiriki ligi kuu msimu uliopita ambao anaona wanaingia katika kikosi chake bora kwa msimu uliomalizika hivi karibuni.
Leo tunaanza na kocha aliyetwaa ubingwa akiifundisha Yanga, Hans van der Pluijm ambaye amewataja wachezaji 11 anaoona wameonesha ubora wa hali ya juu kwenye msimu huu.
“Golini namuweka Ally Mustafa, nadhani amecheza vizuri sana, beki wa kulia ni Juma Abdul, mabeki wa katikati nawaweka Paschal Wawa na Nadir Haroub, kushoto Tshabalala kutoka Simba, sijui jina lake, najua jina lake la utani ni Tshabalala”, amesema Pluijm.
“Safu ya kiungo ni Said Ndemla kutoka Simba, winga wa kulia ni Msuva, winga wa kushoto Emmanuel Okwi, kiungo wa mbele Niyonzima na washambuliaji wawili ni Amissi Tambwe na Kavumbagu”, Pluijm alimaliza kikosi chake.
“Sikuwepo wakati ligi inaanza, nilianza kazi Yanga mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka jana, lakini kwa kipindi nilichoona ligi nimewaona wachezaji hao kuwa bora zaidi msimu huu”, Pluijm alimaliza.
Kwa mujibu wa van der Pluijm, kikosi bora cha msimu uliomalizika wa 2014-2015 kinaundwa na wachezaji wafuatao, kwenye mabano ni timu wanazotokea.
  1. Ally Mustafa ‘Barthez’ (Yanga SC)
  2. Juma Abdul (Yanga SC)
  3. Mohamed Hussein ‘Tshabala’ (Simba SC)
  4. Nadir Haroub ‘Cannavaro’ (Yanga SC)
  5. Paschal Wawa (Azam FC)
  6. Said Ndemla (Simba SC)
  7. Simon Msuva (Yanga SC)
  8.  Haruna Niyonzima (Yanga SC)
  9. Amis Tambwe (Yanga SC)
  10. Didier Kavumbagu (Azam FC)
  11. Emmanuel Okwi (Simba SC)
Tutaendelea kukuletea vikosi vingine kutoka kwa makocha wengine ambao timu zao zimeshiriki ligi kuu ambayo imemalizika hivi karibuni.

clouds stream