Tuesday 2 August 2016

Mkuu Wa Wilaya, Mbunge Arusha Wachongeana Kwa Naibu Waziri


Tarehe August 2, 2016Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Mrisho Gambo.
Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Mrisho Gambo.
Mbunge wa Arusha Mjini, Goodbless Lema amemvaa Mkuu wa Wilaya hiyo, Mrisho Gambo mbele ya Naibu Waziri Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Suleiman Jaffo akidai anaingilia shughuli za halmashauri kinyume na taratibu.
Lema alimtuhumu Gambo kutoheshimu mipaka yake ya kiutawala kwa kuingilia maamuzi ambayo yamejadiliwa kwenye vikao halali vya halmashauri na kupitishwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa katika kikao cha Wakuu wa Idara, Maofisa Tarafa, Waratibu wa Elimu Kata, Watumishi wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka (Auwsa).
Amesema pia amekuwa akiingilia utendaji wa Watumishi wa Halmashauri kwa kuingilia upangaji wa vibanda vya wafanyabiashara kupitia madalali na kusababisha usumbufu na kuongeza kuwa amekuwa akitaka uwanja ulionunuliwa na mfanyabiashara urudishwe Jiji wakati kesi imempa uhalali aliyenunua kuchukua eneo hilo.
“Nimeona nizungumze hapahapa ili naibu waziri ufahamu hali ilivyo hapa. Kwa mfano, Baraza la Madiwani lililopita ndilo lililopitisha kiwango cha posho kwa madiwani kutoka Sh100,000 hadi Sh120,000, jambo la kushangaza DC ameandika barua Tamisemi na nakala kwa Takukuru ili wachunguze jambo ambalo limeshapata baraka za Tamisemi,” alisema Lema.
Hali hiyo ilimfanya Naibu Waziri, Jaffo kuingilia kati na kuahidi kuzishughulikia changamoto hizo na kumpa nafasi Gambo kujibu madai ya Lema ambayo aliyakanusha, likiwamo la kuingilia utendaji kazi wa mamlaka ya maji.
Akijibu tuhuma hizo, Gambo alisema Mheshimiwa mbunge nataka ujue mimi ndiyo mkuu wa shughuli za Serikali hapa wilayani kwakuwa Rais aliona ninafaa ndiyo maana akaniteua na sihitaji na sihitaji kujifunza kazi hii kwani huu ni mwaka wa tano hivyo muda wowote nina uwezo wa kuingilia kati mambo ambayo naona hayaendi sawa hata kama yupo katibu tawala na viongozi wengine.
Baada ya majibizano hayo, Jaffo alimtaka Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Richard Kwitega kushughulikia changamoto hizo akisema muda wa siasa umepita na wananchi wanahitaji maendeleo na kuongeza kuwa Serikali ipo mbioni kuwahamisha watumishi wa Halmashauri ya Jiji wanaofanya kazi kwa mazoea na kumwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Athuman Kihamia kusimamia wafanyakazi wanaofanya kazi kwa mazoea huku wananchi wakipata shida.

clouds stream