Tuesday 2 August 2016

Sabodo Akoshwa Na Magufuli, Asitisha Misaada Chadema


Tarehe August 2, 2016Mfanyabiashara maarufu, Mustapha Jaffer Sabodo wakati alipomkabidhi Mwenyekiti Chadema hundi ya Fedha kusaidia kuimarisha Demokrasia.
Mfanyabiashara maarufu, Mustapha Jaffer Sabodo wakati alipomkabidhi Mwenyekiti Chadema hundi ya Fedha kusaidia kuimarisha Demokrasia. Mfanyabiashara maarufu, Mustapha Jaffer Sabodo ametangaza rasmi kusitisha kukisaidia fedha chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kufuatia kukoshwa na utendaji wa Rais Dkt John Pombe Magufuli.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dares salaam jana , Sabodo alisema atawekeza dola za Marekani bilioni 5 (Sh trilioni 10) mkoani Dodoma, ikiwa ni njia ya kumuunga mkono Rais John Magufuli kuhamisha makao makuu ya serikali kwenda mkoani humo.
 “Huko nyuma nilikuwa nawapa Chadema fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo na kuimarisha demokrasia, sasa natangaza tena kwamba sitawapa tena fedha, niwape za nini wakati Rais aliyeko madarakani anafanya kazi ambayo ndio nilikuwa naipigania” alisema Sabodo.
Sabodo alisema iwapo serikali yote itahamia mkoani humo, itakuwa ametimiza ndoto ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere ambaye alitamani kuona mkoa huo unakuwa makao makuu ya nchi.
Aliongeza alichofanya Rais Magufuli, kimewashinda marais wengine waliomtangulia, hivyo yeye kama mfanyabiashara na mtu mwenye mapenzi makubwa kwa nchi yake, lazima aunge mkono hatua hiyo ya Serikali kuhamia Dodoma ambayo aliita ‘Azimio la Dodoma’.
“Kwa hiyo natangaza kuunga mkono Azimo la Dodoma kwa kuwekeza dola za Marekani bilioni 5, ambazo zitatumika kwa ajili ya uwekezaji mkubwa katika huduma mbalimbali za jamii mkoani humo,” alisema Sabodo.
Kuhusu uwekezaji alisema atawekeza kwenye viwanda kama vya mvinyo, viwanda vya kusindika mihogo na viwanda vingine ambavyo vitahitajika katika mkoa huo.
Sabodo alisema kwamba juhudi zake za kuwekeza katika huduma za jamii kama shule, pia ataziendeleza katika mkoa huo kwa kuhakikisha kwamba zinajengwa shule kadhaa za kisasa, ambazo zitamudu mahitaji ya watu wa eneo hilo.
Kwa upande wa huduma ya afya, Sabodo alisema atatumia umaarufu wake kuwashawishi wamiliki wa Hospitali ya kimataifa ya Apollo ya India ili waje nchini wakashirikiane naye kujenga hospitali ya kisasa, ambayo itakuwa inatoa huduma za kisasa mkoani humo.
Sabodo ni mfanyabiashara wa kitanzania mwenye asili ya Kihindi ambaye alizaliwa mkoani Lindi. Katika maisha yake amekuwa anafanya biashara katika nchi za Kenya, Ufaransa, India, Sudan na Zimbabwe.

clouds stream