Saturday 6 August 2016

UKUTA Sasa Wapigwa ‘STOP’ Dar Baada Ya Mbeya, Iringa.

Tarehe August 6, 2016
1 (1)V 1

Jeshi la Polisi Mkoa wa Dar es Salaam limetakiwa kuhakikisha kwamba sheria zinafuatwa na kusiwepo kitu kinachoitwa UKUTA ili wananchi waendelee na kazi zao kama kawaida.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alipokuwa akizungumza na kikosi cha kutuliza ghasia katika kambi ya Ukonga Jijini Dar es salaam na kuwaambia askari hao wanafahamu sheria hivyo wasisubiri mtu yeyote kuja kuwakumbusha juu ya jambo hilo au maelekezo mengine kwa kuwa Amiri Jeshi ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameshaagiza kinachotakiwa ni utekelezaji.

Amewataka kutosubiri maelekezo yoyote kutoka juu ili asiwepo mtu yeyote atakayelazimika kufunga duka kwa sababu ya UKUTA.

“Nyie ni matrekta hakuna UKUTA unaweza kusimama mbele yenu, mimi kama Mkuu wa Mkoa ninaamini hatutakuwa na vurugu kwenye Mkoa wetu na hatuwezi kuruhusu vurugu kwa kuwa tunajua madhara ya vurugu,’’ amesema.

 Naye Kamanda wa Oparesheni Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Lucas Mkondya amesema jeshi hilo lipo vizuri na vijana wameandaliwa vizuri na wameandaliwa kuwa tayari siku nyingi na hakuna mtu yeyote atakayethubutu kufanya UKUTA na watakaofanya hivyo watazimwa kabla hawajafanya chochote.

Amewataka wananchi wote wa Jiji la Dar es Salaam kutojitokeza kwenye operesheni UKUTA kwa kuwa maandamano hayo siyo halali na watakaojitokeza watapata matatizo yasiyowahusu.

Operesheni UKUTA iliyotangazwa na CHADEMA inatarajiwa kutekelezwa Septemba 1, mwaka huu ambapo wamepanga kufanya maandamano na mikutano nchi nzima.

clouds stream