Thursday 11 August 2016

Stendi Kuu Ya Mabasi Kuhamia Mbezi Mwisho, Kufanywa Ya Kimataifa

Tarehe August 11, 2016
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.V 1

 Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema kuwa Serikali ipo katika mpango wa mwisho wa kuihamishia stendi kuu ya mabasi kutoka Ubungo kwenda Mbezi Mwisho ili kuwa na stendi ya kimatatifa tofauti na ya sasa.

Amesema pamoja na mambo mengine sababu za kuhamishwa kwa stendi hiyo ni kuepuka kero ya kukutana na mabasi ya mwendo kasi kwakuwa nayo ni moja ya changamoto kubwa katika stendi kuu ya mabasi Ubungo.

Mhe. Makonda aliyasema hayo katika ziara ya ghafla aliyoifanya katika stendi ya Ubungo kwa lengo la kujionea hali ya sasa na stendi hiyo kuu.

Aidha, amewapiga marufuku mawakala wanaotoza faini za kuegesha magari vibaya katika Kituo Kikuu cha Mabasi yaendayo Mikoani cha Ubungo hadi hapo yatakapotengenezwa maeneo rasmi kwa ajili ya maegesho ya magari.

Amesema haiwezekani mawakala wakaendelea kutoza faini za maegesho ambayo si sahihi wakati katika eneo hilo hakuna maeneo maalumu kwa ajili ya maegesho ya magari.

“Nataka maeneo rasmi yakishatengwa ndipo muanze kutoza faini, mmekuwa mkiwasumbua wananchi hawajui wapi ni sehemu ya maegesho na wapi si sehemu ya maegesho wekeni alama ndipo muanze kuwatoza,” ameongeza Makonda.

Wakati huohuo amemtaka Mkurugenzi wa Jiji kuhakikisha kituo hicho kinawekwa taa ili kuondoa usumbufu wanaokutana nao abiria na wananchi hasa wakati za usiku kabla ya kumalizika wiki hii na kuahidi kurejea baada ya siku 20 kujionea utekelezaji wa agizo hilo.

“Shahuku yangu ni kuwa na stendi tofauti na tuliyonayo, nataka Dar es salaam iwe na stendi ya kimataifa na tayari tunalo eneo kule mbezi ambapo halmashauri ya Jiji tayari ipo kwenye mchakato wa kukamilisha ujenzi huo.

clouds stream