Wednesday 3 August 2016

Rais Magufuli Kuongoza Vijana Kuadhimisha Siku Yao.

Tarehe August 4, 2016
1 (1)
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. John Pombe Magufuli anatarajiwa kuwa Mgeni rasmi siku ya Kilele cha maadhimisho ya siku ya Vijana Kitaifa yatakayofanyika Mkoani Simiyu Oktoba 14 mwaka huu.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Vijana Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Antony Mavunde amesema kuwa Kauli mbiu ya Siku ya Vijana mwaka huu ni “Tokomeza umasikini kwa uzalishaji endelevu na matumizi yenye tija”.
Amesema lengo la kauli mbiu hiyo ni kuzihimiza nchi wanachama wa umoja wa mataifa kushirikisha kikamilifu Vijana katika shughuli za uzalishaji na kuhakikisha kuwa panakuwepo na matumizi sahihi ya rasilimali za nchi kama vile ardhi,maji,madini na Nishati ili kufikia shabaha ya kuwa na maendeleo endelevu ifikapo 2030.
Akizungumzia maadhimisho hayo Kitaifa Mhe . Mavunde alisema kuwa vijana watapata fursa ya kushiriki shughuli mbalimbali kama makongamano, matamasha, michezo, maonyesho ya Kazi za Vijana, shughuli za kujitolea na maandamano ya amani.
“Tanzania tutasherekea siku ya Vijana Duniani Kitaifa kuanzia tarehe 8/10/2016 na kilele kitakuwa tarehe 14/10/2016 Mkoani Simiyu ambapo Sherehe hii itaenda sambamba na Maadhimisho ya kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere, Wiki ya Vijana Kitaifa na kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2016.” amesisitiza Mhe. Mavunde.
Wazo la kuwa na siku ya Vijana Duniani lilitolewa katika Mkutano wa Vijana wa Kimataifa mwaka 1991 Mjini Vienna Australia kwa madhumuni ya kutafuta njia ya kuchangisha fedha za kusaidia mifuko ya Taifa ya Vijana ambapo mwaka 2000 nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa ikiwemo Tanzania zilianza kuadhimisha siku ya Vijana Duniani kulingana na mazingira yake kwa kuzingatia kauli mbiu ambayo huandaliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa

clouds stream