Monday 16 March 2015

Mashali aendeleza ubabe, amsulubu Dullah Mbabe

Mashali aendeleza ubabe, amsulubu Dullah Mbabe


Thomas Mashali (kulia) akimuadabisha Dullah Mbabe jana usiku, Mashali alishinda kwa pointi za majaji wawili kwa mmoja
Thomas Mashali (kulia) akimuadabisha Dullah Mbabe jana usiku kweye pambano lao la raundi 10, Mashali alishinda kwa pointi za majaji wawili kwa mmoja
Bondia wa ngumi za kulipwa nchini, Thomas Mashali ‘Simba asiyefugika’ jana usiku alimtwanga Abdallah Paazi ‘Dulla Mbabe’ kwa ushindi wa pointi kwenye pambano la raundi 10 ambalo halikuwa la ubingwa lililopigwa kwenye viwanja vya ndani vya Taifa.
Pambano hilo lililokuwa kali na lenye kuvutia, lilianza kwa kasi huku Mashali akianza vyema pambano hilo kwa kumsukumia makonde mazito mpinzani wake kwenye raundi za mapema. Mbabe nae hakuwa nyuma kwani alikuwa akijibu mapigo na kulifanya pambano hilo kuwa la kuvutia zaidi.
Mashali ambaye ni mzoefu kwenye mchezo wa masumbwi, alionekana kuchachamaa kuanzia raundi ya saba na kubadilisha kasi ya mchezo kitu ambacho kilimchanganya Mbabe aliyeonekana kupungua kasi kadri muda ulivyokuwa unayoyoma.
Wakali hao walitambiana kabla ya pambano lao hali iliyopelekea kutaka kuzichapa ‘kavukavu’ siku ya Jumamosi walipokutana kwenye zoezi la kupima uzito kabla ya pambano lao la jana.
Kwenye mapambano mengine ya utangulizi, Japhet Kaseba alikubali kichapo kutoka kwa bondia Said Mbelwa, mpambano uliokuwa wa raundi nane ambapo Mbelwa alishinda kwa pointi za majaji wa wili kwa mmoja.
Pambano jingine la raundi 10 liliwakutanisha Mada Maugo dhidi ya Karama Nyilawila ambapo Maugo aliibuka mshindi kwenye pambano hilo kwa pointi za majaji wawili kwa mmoja na kukata ngebe za nani mkali wa kutupa makonde kati yao.
Pambno jingine la masumbwi la kimataifa litapigwa kati ya Mohamed Matumla ‘Matumla Jr’ dhidi ya Wang Xin Hua kutoka China, pambano hilo litachezwa Machi 27 kwenye ukumbi wa Diamond Jubelee jijini Dar es Salaam.
Pambano hilo litakuwa la uzito wa Super Bantam kuwania nafasi ya kwenda kugombea ubingwa wa taji la dunia la WBF kwenye mapambano ya utangulizi Mei 2 mwaka huu huko Las Vegas Marekani siku ambayo kutakuwa na pambano la Floyd Mayweather dhidi ya Manny Pacquiao.

clouds stream