Thursday 26 March 2015

Watu 2 Wakamatwa na Mifupa ya Albino Kagera

Watu 2 Wakamatwa na Mifupa ya Albino Kagera


Jeshi la Polisi mkoani Kagera  linawashikilia  watu 2  kwa kosa la kukutwa na viungo mbalimbali vya mwili ikiwemo mifupa mitatu ya mtu mwenye ulemavu wa ngozi (albino).
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani Kagera Henry Mwaibambe alisema kuwa tukio hilo limetokea juzi katika kijiji cha Kyota kata ya Kimwani wilayani Muleba mkoani Kagera baada ya jeshi hilo kuweka mtego kwa watuhumiwa hao ambao walikuwa wanatafuta wateja wa viungo hivyo.
Watuhumiwa waliokamatwa  ni James Rutozi (66) mkazi wa Kimwani ambaye ndiye aliyekuwa anahifadhi viungo hivyo na Emanueli Kaloli (50) ambaye pia ni mkazi wa Kimwani aliyekuwa anatafuta mteja wa viungo hivyo.
Jinsi  watuhumiwa hao walivyokamatwa,
Alisema mara baada ya kupata taarifa kuwa kuna watu wanauza viungo hivyo kwa Sh milioni 3 waliweka pesa za mitego na kujifanya wao ni wateja na ndipo walipowakamata watuhumiwa hao wawili ambao walikutwa na mfupa mmoja na walipowabana zaidi ndipo walitoa mifupa miwili.
Mnamo mwaka 2006 katika kijiji cha Rushwa kata ya Mushabago wilayani Muleba, Zeulia Jestus akiwa na miaka 24 mwenye ulemavu wa ngozi (albino) alifariki dunia muda mfupi baada ya kujifungua na ndipo watuhumiwa hao walifukua kaburi hilo mwaka 2008 kwa maelekezo ya mganga wa jadi.
Ameongeza kuwa  walipotaka kujiridhisha jeshi hilo liliomba kibali mahakamani ili kufukua kaburi hilo mnamo Machi 23, mwaka huu lilipofukuliwa liligundulika kuwa viungo hivyo vimetolewa katika mwili wa marehemu huyo.
Kwa upande mwingine jeshi la Polisi linamtafuta mganga wa jadi aitwaye Mutalemwa Revocatus ambaye ametoroka kabla kukamatwa. Mganga huyo   ndiye  anayedaiwa kuwashawishi wafukue hilo kaburi na kuwapa dawa ya kinga ili wasidhurike wakati wanafukua.

clouds stream