Monday 8 February 2016

Mawaziri Yona, Mramba Waanza Usafi Hospitali Sinza

Mawaziri Yona, Mramba Waanza Usafi Hospitali Sinza

Tarehe February 8, 2016
Yona na Mramba wakiwa wamevaa mavazi maalum kwa ajili ya kufanyia usafi
Waliokuwa wawaziri wastaafu, Basil Mramba na Daniel Yona leo wameanza kutumikia adhabu ya kifungo cha nje, kwa kufanya usafi katika Hospitali ya Sinza, Palestina, ya jijini Dar, kulingana na hukumu iliyotolewa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wiki iliyopita kuhusu kesi iliyokuwa ikiwakabili.
Mramba aliwahi kuwa Waziri wa Fedha na Yona aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini waliwasili hospitalini hapo majira ya saa 3:30 asubuhi ili kuanza kutumikia adhabu hiyo kama mahakama ilivyowaamuru.
Ofisa huduma za jamii, Deogratius Shirima amewaambia wanahabari na wananchi waliokuwa hospitalini hapo kuwa leo ilikuwa ni siku ya kuwapa maelekezo namna ambavyo watafanya usafi, maeneo ya kufanya usafi pia walikabidhiwa vifaa watakavyovitumia kufanyia usafi kuanzia kesho.
Afisa Mazingira hospitalini hapo, Miriam Mongi, aliwakabidhi Yona na Mramba vifaa vya kufanyia usafi ambavyo ni; mifagio, mafyekeo, viatu vya kufanyia usafi maarufu kama “gambuti” na glovusi.
Mawaziri hao wa zamani walikuwa wanatumikia kifungo cha miaka miwili jela kwa kosa la uhujumu uchumi na ya kuisababisha serikali hasara. Walibadilishiwa adhabu ya jela na kupewa adhabu ya kutumikia kifungo cha nje mwishoni mwa wiki iliyopita.

clouds stream