Tuesday 22 March 2016

Mabasi Yaendayo Kasi Kuanza Majaribio Ndani Ya Wiki Moja-Majaliwa

Tarehe March 22, 2016
10262227_717689465039977_2529648417247638500_n
10262227_717689465039977_2529648417247638500_n
Wazir Mkuu, Kassim Majaliwa amesema mabasi yaendayo kasi (DART) yataanza kufanyiwa majaribio ndani wiki moja kuanzia sasa ili madereva waanze kuzoea njia na taa za kuongozea magari.
Majaliwa ametoa kauli hiyo leo wakati alipofanya ziara ya ghafla katika Soko la Kimataifa la Samaki la Feri iliyokuwa na lengo la kuangalia mfumo wa majiko ya gesi sokoni hapo na kukagua ujenzi wa ukuta unaotenganisha soko hilo na mabasi yaendayo kasi.
Amesema wataanza na mabasi kati ya 30 – 50 ambayo yatapita kwenye njia zote za mradi huo na zoezi hilo litafanyika ili watumiaji wengine wakiwemo waendesha daladala, bodaboda na watembea kwa miguu waweze kutambua kuwa njia ya mabasi yaendayo kasi si ya kwao hivyo waanze kuzoea.
Waziri Mkuu ambaye ametembelea soko hilo kuanzia saa 5:10 hadi saa 5:54, alitoa jibu hilo wakati akijibu maombi ya mfanyabiashara mmoja, Bw. Sharifu Ramadhani ambaye alisema wanatumia fedha nyingi kwa ajili ya usafiri kwa vile mabasi mengi yanaishia Mnazi Mmoja.
“Mabasi yanaishia Mnazi Mmoja na huku ni mbali kwa hiyo tunalazimika kutembea kwa miguu kwa sababu kukodi taxi ni gharama kubwa,” alisema Ramadhani.
Akifafanua kuhusu hatua iliyofikiwa kwenye utekelezaji wa mradi huo, Waziri Mkuu amesema hivi sasa wanakamilisha ufungaji wa mitambo ya kukatia tiketi ambapo abiria atakuwa na kadi kama za benki ambayo anaijaza fedha halafu anapita kwenye mashine, kiasi cha nauli kinakatwa halafu anaingia kwenye basi, hakutakuwa na muda wa kukata tiketi.”
Amesema tatizo la usafiri kwa wafanyabiasha wa feri litakwisha hivi karibuni baada ya mabasi hayo kuanza.

clouds stream