Tuesday 22 March 2016

Majaliwa Amtaka CAG Kukagua Mchezo Kati Ya TPA Na CRDB

Majaliwa Amtaka CAG Kukagua Mchezo Kati Ya TPA Na CRDB

Tarehe March 22, 2016

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) aende Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ili akague taarifa za mapato ambazo zilikuwa zikilipwa na mawakala wa forodha na bandari kupitia benki ya CRDB lakini hazionekani kwenye mifumo ya benki.
Majaliwa ametoa agizo hilo wakati akizungumza na mamia ya mawakala wa forodha na bandari waliohudhuria mkutano aliouitisha ili kusikiliza kero zinazowapata katika utendaji kazi wao.
Akizungumza na mawakala hao kwenye ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu amesema kuna kila dalili za kutupiana lawama baina TPA na CRDB kuhusu malipo yaliyokuwa yakifanyika kibenki lakini fedha hazionekana na wakaati huohuo wakala anaambiwa kuwa hajalipia mzigo wakati alishaulipia.
“Kimsingi bado liko tatizo baina ya Mamlaka ya Bandari pamoja na Benki ya CRDB. Naona kila mmoja hapa anamkana mwenzake. Nitamtuma CAG ili akafanye ukaguzi wa kina ili tujue ni nani kati yao amehusika na upotevu wa fedha,” alisema Majaliwa.
Majaliwa pia amemwagiza Kaimu Mkurugenzi wa Bandari, Injinia Aloyce Matei kuandaa dispatch zote walizotumia kupokelea malipo ya kuanzia mwaka 2015 na ikibidi aandae za kuanzia mwaka 2014 ili CAG atakapozipitia aweze kupata picha halisi.
Vilevile, Waziri Mkuu alimwagiza Injinia Matei kuhakikisha wananunua mashine ya photocopy ili iwekwe kwenye chumba cha kupokelea stakabadhi za malipo ya benki (bank pay in slip) ili mteja anapoleta nakala ya benki aweze kutolewa photocopy na kubakia na nakala ya malipo aliyofanya.
Waziri Mkuu alisema Serikali inatambua bandari ni eneo nyeti katika kuinua uchumi na mapato ya nchi lakini pia ni eneo muhimu katika kutengeneza ajira.
“Ninapenda niwahakikishie kuwa bado tutaendelea kukagua bandari hadi pawe safi kwasababu hii bandari ni yenu na mtafanya kazi kama kawaida,” alisema.
Mapema, akizumgumza kwa niaba ya mawakala hao, Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha nchini (TAFFA), Bw. Stephen Ngatunga alieleza matatizo mbalimbali ambayo wao kama mawakala wa forodha wamekuwa wakikumbana nayo kuanzia ulipaji, utoaji wa mizigo na kuitaka Serikali iongeze nguvu katika kuikabilia sekta hiyo.
Alizikosoa baadhi ya sheria ambazo zinaruhusu wamiliki wa bandari kavu kumiliki pia makampuni ya uwakala wa forodha, sheria kadhaa zinazochangia kukwamisha utoaji wa mizigo bandarini, ukaguzi hafifu wa kwenye scanner na uwepo wa vituo vinane vya mizani kuanzia Dar es Salaam hadi Tunduma ambavyo vimegeuka kuwa kero kwa wasafirishaji wa mizigo kwenda nchi jirani.
Wakati huohuo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Injinia Edwin Ngonyani amesema Serikali imeamua kuyafungulia makampuni zaidi ya 150 ambayo yalikuwa yamefungiwa kufanya kazi za uwakala wa forodha kutokana na madai ya kuhusishwa na ukwepaji wa kodi.

clouds stream