Sunday 6 March 2016

Walimu Mbaroni Kwa Kufanya Mapenzi Na Wanafunzi

Walimu Mbaroni Kwa Kufanya Mapenzi Na Wanafunzi

Tarehe March 5, 2016
Walimu waliofanya mapenzi na wanafunzi wakiwa chini ya ulinzi.
Walimu waliofanya mapenzi na wanafunzi wakiwa chini ya ulinzi.
Walimu wanane wa Shule ya Sekondari Mihama, Kata ya Kitangili, Wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza akiwemo Mkuu wa Shule, wamesimamishwa kazi huku watano kati yao wakishikiliwa na polisi kwa tuhuma za kufanya mapenzi na wanafunzi kufuatia ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo.
Mulongo pia amevunja bodi ya shule hiyo baada ya kubainika kutofanya kikao hata kimoja tangu ilipoteuliwa Aprili 24, 2013.
Mkuu wa Shule hiyo Joseph Malifedha na walimu wengine waliotiwa mbaroni ni Rodrick Uroki, Denis Sanga, Edmund Boaz, Steven Samuel.
Walimu wengine watatu waliokuwa wakifundisha shuleni hapo, lakini wakahamishwa na hivi sasa wanasakwa na polisi kwa tuhuma hizo ni Joseph Lamongi na Joeza Mzava waliohamia Sekondari ya Sangabuye pamoja na Abdallah Mtelwe aliyehamia Tanga.
Malifedha anadaiwa kuwachangisha fedha wanafunzi wa kidato cha kwanza na cha tatu kwa ajili ya picha za kuweka kwenye vitambulisho (passport size).
Akitangaza uamuzi huo, Mulongo alisema tume maalumu ya uchunguzi iliyoundwa Januari 27, kuchunguza tuhuma dhidi ya walimu hao kujihusisha na mapenzi na wanafunzi imebaini ukweli baada ya kuwahoji wanafunzi kadhaa.
“Ni fedheha na haivumiliki kuona walimu wakifanya mapenzi na wanafunzi wao. OCD wakamate walimu wote na uanze uchunguzi mara moja na kukusanya ushahidi utakaowezesha wahusika kufikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake,” aliagiza Mulongo.
Amri hiyo ilitekelezwa mara moja kwa walimu hao kuwekwa chini ya ulinzi.
Mulongo pia alimwagiza Katibu wa Idara ya Utumishi wa Walimu Mkoa wa Mwanza, Genzi Sahani kuwaandikia barua za onyo walimu wa kike shuleni hapo kwa kushindwa kulinda na kutetea masilahi ya wanafunzi wa kike waliokuwa wakidhulumiwa kingono na walimu wenzao kiasi cha baadhi yao kuathirika kisaikolojia.
Pia, alimwagiza Ofisa Elimu Mkoa wa Mwanza, Khamisi Maulid kuangalia uwezekano wa kuwahamishia shule nyingine wanafunzi waliodhulumiwa kingono na walimu wao ili kuwaepusha na matatizo ya kisaikolojia.
Maulidi alisema wanafunzi walioathirika zaidi ni wale wa kidato cha nne.
Katibu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Mkoa wa Mwanza, Said Mselem alisema kitendo hicho kimeifedhehesha taaluma ya ualimu na kuahidi kuwa ofisi yake itatanua wigo wa uchunguzi hadi kwenye shule nyingine.

clouds stream