Friday 4 March 2016

Msiharibu Kazi Mkitegemea Uhamisho-Waziri Mkuu Aonya

Msiharibu Kazi Mkitegemea Uhamisho-Waziri Mkuu Aonya

Tarehe March 4, 2016
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema watumishi wa umma wako huru kuhamia kokote wapendako lakini wahakikishe wanaenda huko wakiwa safi na kamwe mtu asiharibu kazi akitarajia kuwa atahamishiwa sehemu nyingine.
Majaliwa ametoa onyo hilo leo wakati akizungumza na watumishi wa Wilaya ya Itilima kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo ambao ameuzindua leo Mkoani Simiyu.
Amesema Serikali hii haina utumishi kwa mtu aliyeharibu kazi. Usije ukaharbu hapa Itilima ukadhani utaenda Bunda kuendelea na kazi. Serikali ya awamu hii haina nafasi na watumishi wa aina hiyo.
“Watumishi wenzangu huu ni wakati wa kubadilika na kuona mwelekeo wa Serikali hii ya Awamu ya Tano ukoje na jukumu letu ni kuwatumikia Watanzania wote bila kujali itikadi zao, rangi wala dini zao,” amesema.
Waziri Mkuu aliwahakikishia watumishi hao kwamba Serikali inatambua changamoto walizonazo kutokana na upya wa Wilaya hiyo na Mkoa huo na akawaahidi kuwa  mazingira Yao yataboreshwa.
“Msiwaadhibu wananchi kwa kisingizio cha mazingira magumu ya kazi zenu, tunajua mnayo madai ya nauli, posho za mafunzo, kupandishwa madaraja na malimbikizo ya likizo,” alisema huku akishangiliwa.
Alisema Serikali itayalipa madeni hayo japo haitamaliza yote kwa wakati mmoja ila ana uhakika wa kukamilisha walau kwa asilimia 80.
Mapema akitoa taarifa Mkuu wa Wilaya hiyo, Bibi Georgina Bundala alisema wilaya hiyo iliyoanzishwa Machi, 2012 na kupata Halmashauri Julai 2013 haina kituo cha polisi cha wilaya, haina gereza, ofisi za TAKUKURU, mahakama ya wilaya, hospitali ya wilaya wala benki.

clouds stream