Tuesday 19 July 2016

Hatupokezani Vijiti Bali Tunachagua Mwenyekiti Wa CCM-Ole Sendeka


Tarehe July 19, 2016ccm
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kwamba Mkutano Mkuu Maalumu wa chama hicho unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni sio wa kupokezana vijiti, kwa sababu nafasi za Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti unapofika wakati wa uchaguzi haziombwi, bali yanapendekezwa majina ya watu wanaofaa kushika nyadhifa huo na kuteuliwa.
Hayo yamesemwa na Msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka na kusema kama atachaguliwa, Rais Magufuli atakuwa Mwenyekiti wa CCM wa tano baada ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Kikwete.
“Kwa mujibu wa Katiba ya CCM, nafasi ya Mwenyekiti wa CCM na Makamu Mwenyekiti wawili unapofikia wakati wa uchaguzi nafasi hizi haziombwi isipokuwa Kamati Kuu inafikiria na kupendekeza majina na kuyawasilisha kwa Halmashauri Kuu ya Taifa ambayo humteua,” amesema Sendeka.
Amesema baada ya hapo Mkutano Mkuu wa Taifa unamchagua kwa kumpigia kura na kuongeza kuwa wanaopendekezwa hawajazi fomu za kugombea nafasi hizo na katika mchakato huo kinachofanyika si kupokezana kijiti, kama wengi wanavyopenda kuita, bali ni uchaguzi wa kumpata mwenyekiti wa CCM.
“Katika uchaguzi huo itapigwa kura ya ‘ndio’ au ‘hapana’ ili kupata mwenyekiti na lazima apate nusu ya kura na akipata chini ya nusu mapendekezo yataanza upya,” ameongeza Sendeka.
Mkutano huo unatarajiwa kushirikisha wajumbe 2,456 na mpaka sasa wamekodi hoteli 306 ambazo zitawalaza zaidi ya watu 3,331 mjini Dodoma.
Viongozi watakaojiuzulu ili kupisha Dkt. Magufuli kupanga safu yake mpya ya uongozi ni pamoja na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, Manaibu Katibu Wakuu wawili na watendaji wengine.
Wajumbe wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa ni pamoja na Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu Bara, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Katibu wa Oganaizesheni, Katibu wa Siasa na Uhusiano ya Kimataifa, Katibu wa Uchumi na Fedha na wa Itikadi na Uenezi.
“Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana atakabidhi barua yake kwa mwenyekiti wa chama kupisha Rais Magufuli aweze kuunda safu yake ya watu atakaofanya nao kazi,” amesema Sendeka na kuongeza kuwa anaamini Magufuli ataunda safu nzuri itakayoleta mabadiliko.

clouds stream